Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, leo, anatarajia
kujua hatima ya dhamana ya kesi ya uchochezi inayomkabili.
Lema anashikiliwa katika mahabusu ya Magereza ya Kisongo mjini
Arusha.
Wakili wake, Peter Kibatala amesema walikata rufaa chini ya hati
ya dharura kuomba Mahakama isikilize kesi hiyo mapema.
Amesema waliamua kufuata maelekezo ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sekela Mosha ya kuwataka kukata rufaa.
Katibu wa mbunge huyo, Innocent Kisanyage amesema rufaa hiyo
itasikilizwa leo saa tatu asubuhi baada ya kukamilisha mambo yanayotakiwa.
Lema alirudishwa mahabusu kutokana na Mahakama Kuu Kanda ya
Arusha kukataa kupokea ombi lake la kufanya marejeo ya uamuzi wa kunyimwa
dhamana.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mosha alisema uamuzi
uliofanywa na Mahakama ya Hakimu Mkazi umeegemea kifungu cha Sheria cha Makosa
ya Jinai CPA 148, hivyo kilimtaka mshtakiwa kukata rufaa siyo kuomba Mahakama
hiyo kufanye rejea,
Rufaa hiyo itasikilizwa na Jaji Fatuma Massengi, huku Lema
akitimiza siku ya 26 tangu apelekwe Gereza la Kisongo.
No comments:
Post a Comment