Serikali imetakiwa kuangalia upya tozo za magari ya watumishi wa
serikali wakati wa kuvuka daraja la Nyerere lililopo Wilaya ya Kigamboni jijini
Dar es Salaam.
Mkuu
wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, ameyasema hayo leo katika ziara ya
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ya kuangalia na kutatua changamoto
za wananchi wa eneo hilo.
Alilitaka Shirika la Hifadhi ya
Jamii (NSSF) kuangalia upya tozo hizo za magari ya Halmshauri hiyo na watumishi
wa umma wanaoishi nje ya Halmshauri kutozwa fedha kuvuka katika daraja hilo
jambo ambalo linaleta changamoto kubwa kwa na kuwaongezea sababu.
“Kila gari ya Halmashari inayopita
katika daraja hili inatozwa fedha ya shilingi 2000,hasa ikizingatiwa kuwa
halmashauri hii ni mpya hivyo watumishi wengi wanatokea nje ya
halmashauri,”alisema.
Akitoa ufafanuzi kuhusu suala la
tozo la daraja hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Profesa Godius Kahyrara, alikiri
kupokea malalamiko ya watu wengi kutaka kupunguziwa au kuondolewa tozo hiyo.
“Ni kweli tumekuwa tukipokea
malalamiko hayo kutoka kwa wananchi mbalimbali, lakini suala ni kwamba sisi
kama NSSF huwa hatupangi viwango vya tozo za kuvuka daraja bali tunapokea
maelekezo kutoka wizara husika (Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi),”alisema.
Aliongeza kuwa atawasilisha suala
hilo katika wizara husika ili kuona uwezekano wa kuondoa tozo hiyo ama
kupunguza.
Kahyarara alitaja changamoto
zingine kuwa ni uwepo wa vijana kuligeuza daraja hiyo kuwa kijiwe na wengine
kuwa na nia ovu ya kulihujumu kwa kuharibu miundombinu, ingawa ulinzi
umeendelea kuimarishwa.
Kwa
upande wake RC Makonda amesema chanzo cha magari ya Halmashauri hiyo kutozwa
tozo ni kutokana na mchakato na ujenzi wa daraja hilo kufanyika kabla ya
Halmshauri ya Manispaa ya Kigamboni kuanzishwa.
Katika hatua nyingine DC Mgandilwa
alimuomba RC Makonda kuangalia uwezekano wa kuunganisha barabara ya vumbi eneo
la Vijibweni kutoka daraja la Nyerere lenye urefu wa kilometa 1.5 ili kuondoa
adha ya wananchi wanaotumia barabara hiyo.
“Hii barabara licha ya kutumiwa na
magari mengi yanayopita katika daraja hili, lakini haijajengwa kwa kiwango cha
lami hivyo wananchi kupata kero kubwa kutokana na vumbi na magari kugonga mawe
tunaomba utusaidie,”alisema Mgandilwa.
Akihutubia wananchi wanaoishi
karibu na mradi wa daraja hilo,RC Makonda amewahikishia kuwa barabara hiyo
itaanza kujengwa baada ya wiki mbili ili kuondoa changamoto wanazokutana nazo
wananchi.
No comments:
Post a Comment