Hatma ya dhamana ya Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), ilishindwa kujulikana jana baada ya
mawakili wa Serikali kuweka pingamizi, wakipinga Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha
kusikiliza maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na mawakili wa mshtakiwa.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama
hiyo, Jaji Sekela Moshi, alisema kutokana na pingamizi hiyo,
atasikiliza hoja za sheria zilizowasilishwa mahakamani hapo kabla hajatoa
uamuzi wowote juu ya dhamana ya mshtakiwa.
Aliwaelekeza mawakili wa pande zote
mbili kuwasilisha hoja za sheria kabla mahakama haijaendelea na hatua yoyote.
Jaji Moshi alisema atatoa uamuzi
kuhusu mvutano huo wa sheria, Novemba 22, mwaka huu
Katika maombi hayo namba sita ya
mwaka 2016, Jamhuri iliwakilishwa na mawakili, Matenus Marandu na Paul Kadushi
wakati Lema anatetewa na jopo la mawakili sita ambao ni Peter Kibatala, John
Mallya, Adam Jabir, Sheck Mfinanga, Faraji Mangula na Charles Adiel.
Katika shauri hilo jana, hoja za
sheria za pingamizi zilianza kusikilizwa saa 4:54 asubuhi hadi saa 7:25 mchana
ambako mawakili wa Serikali na wale wa upande wa utetezi, walichuana vikali
kujenga hoja.
Akiwasilisha pingamizi hilo, wakili
Kadushi, aliiomba mahakama iwaruhusu kuwasilisha pingamizi moja na kama
mahakama ikishindwa kuridhia pingamizi hilo, wawasilishe pingamizi la pili.
Alidai maombi hayo
yaliyosainiwa na wakili Kibatala yanalenga katika kifungu cha 372 (1) cha
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinachoipa Mahakama Kuu kufanya mapitio
ya mashauri ya kesi za mahakama za chini.
Alidai hoja ya sheria
inasema mabadiliko ya sheria yaliyofanyika mwaka 2002 yaliondosha
haki za pande zote katika kesi za jinai kuomba rufaa au mapitio ya uamuzi mdogo
uliofanywa katika mahakama zinazoongozwa na mahakimu nchini.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 43 (2)
cha sheria ya mahakama za mahakimu, maombi hayo yanakinzana na kifungu hicho
kwani uamuzi huo mdogo unaopingwa na mawakili wa mshtakiwa, haujamaliza shauri
la jinai.
“Lakini pia, uamuzi huo
unaobishaniwa na mawakili wa mshtakiwa, uko katika ukurasa wa 17 hadi 19, hivyo
mahakama inafungwa na sheria kusikiliza rufaa au mapitio katika uamuzi mdogo.
“Kwa kuwa uamuzi ni mdogo mahakama
inakuwa na uamuzi wa kutupilia mbali maombi haya na kusubiri tuendelee na
mwenendo wa kesi. Lakini, kama mahakama haitavutiwa au kushawishiwa na
hoja hii, tunaomba kutoa hoja ya pili,”alidai wakili Kadushi
Baada ya hatua hiyo, hoja ya pili
iliwasilishwa ikisema maombi ya Lema hayajakidhi matakwa ya sheria, kifungu cha
359 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20 kama
ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2,002.
Kwa mujibu wa wakili Kadushi,
kifungu hicho kinaelekeza namna mtu asiporidhika na uamuzi uliotolewa na
mahakama ya chini, anavyotakiwa kukata rufaa mahakama kuu.
“Msingi wa sheria umeshawekwa na
mahakama kuwa maombi ya kufanya mapitio kamwe siyo mbadala wa rufaa na uamuzi
mwingi umetamka hivyo,” alidai wakili Kadushi.
Katika maelezo yake, wakili huyo
alirejea mashauri mbalimbali ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa yenye kesi za
namna hiyo na kudai kuwa kulikuwa na haki ya waleta maombi kukata rufaa na haki
hiyo ipo mpaka sasa.
Wakili Kibatala
Kibatala ambaye alikuwa akiwawakilisha
mawakili wenzake watano, alidai hoja za sheria zilizowasilishwa
mahakamani hapo na upande wa Jamhuri hazina msingi katika sheria na akaiomba
mahakama izitupilie mbali.
Aliiambia mahakama
kwamba hakimu aliyeruhusu wakili wa Serikali kusimama kabla hajafikia mwisho wa
uamuzi aliokuwa akiusoma ni ishara kuwa mahakama hiyo haikuongozwa vizuri jambo
ambalo linaifanya Mahakama Kuu iingilie kati na kutoa maelekezo.
“Hoja walizoleta Serikali
hazijakidhi matakwa ya sheria. Kwanza kabisa, pingamizi lao halijasema linakuja
kwetu au linakwenda kwa mahakama kwa sababu sisi na Serikali tumeitwa hapa
mahakamani na hii ni kama mwananchi wa kawaida kwenda kwa msajili kulalamika
kisha jaji akaziiita pande zote mahakamani,” alisema Kibatala.
Alisema wanaishangaa Serikali
kuzungumzia kifungu cha 43 ambacho barua ya maombi yao haijakizungumza na pia
mahakama kuitisha majalada na kupitia yaliyotokea mahakama za chini, inajenga
mamlaka na kuruhusu mahakama kuu kuitisha majalada hayo kupitia mwenendo au uamuzi.
“Kifungu cha 373 cha sheria hiyo ya
makosa ya jinai, kinaelezea jinsi Mahakama Kuu inavyoweza kupata taarifa ya
upungufu wa mwenendo katika mashauri yanayoendelea mahakama za chini.
“Mfano mahakama za chini
zinaruhusiwa zenyewe kupeleka majalada mahakama kuu ili kupitia mwenendo au
kupata taarifa yoyote au kuomba namna ya kurekebisha wanapokosea na hata
mwanasheria mkuu wa Serikali amewahi kutumia mfumo huu katika kesi mbalimbali,”alisema Kibatala.
Alisema mahakama kuu ina mamlaka ya
kupokea malalamiko na kuyafanyia kazi na ina uhuru wa kuitisha majalada na
kusikiliza maombi ya upande wowote kati ya Serikali au utetezi.
Katika maelezo yake, Kibatala
alisema kifungu cha 148 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinasema
rufaa inaweza kukatwa kama mtu amenyimwa dhamana ila uamuzi wa mtu kunyimwa
dhamana haukatazi mshitakiwa kuomba mapitio ya uamuzi huo.
“Mahakama ilijivua mamlaka ambayo
inayo ikiwa ni pamoja na kazi yake ya sheria. Katika hili, hakimu alikosea
kumruhusu wakili wa Serikali kusimama katikati ya uamuzi.
“Nasema hivyo kwa sababu kifungu
cha 148 (6) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinasema mahakama ikitoa
dhamana kwa mshitakiwa ni lazima ifikie mwisho wa hatua ya uamuzi wake kwa
kuweka masharti ya dhamana.
“Lakini katika suala hili, mahakama
iliishia njiani baada ya wakili wa Serikali kuingilia kati na kueleza kusudio
la kukata rufaa.
“Jukumu letu ni kuiongoza mahakama
na siyo kuviziana ili tushinde. Hapa Kadushi amedai haturuhusiwi kuomba mapitio
au rufaa ila akasema tulipaswa kukata rufaa na siyo kuomba mapitio ya mwenendo
wa uamuzi ule.
“Kwa misingi hiyo, ndiyo maana
tunasisitiza kwamba pingamizi la Jamhuri halina mashiko yoyote ya sheria,
tunaomba litupiliwe mbali na mahakama isikilize maombi yetu,” alisema Wakili
Kibatala.
Katika maombi hayo, Lema kupitia
mawakili wake, anaiomba mahakama hiyo ifanye mapitio ya majalada ya kesi za
jinai namba 440 na 441 ya mwaka huu ambako anakabiliwa na makosa ya uchochezi
dhidi ya Rais Dk. John Magufuli
Mawakili hao wa Lema wanaomba ombi
hilo kwa sababu wakati Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Desderi
Kamugisha akisoma mwenendo wa uamuzi huo uliokuwa na kurasa 22 hivi karibuni,
alisema mahakama hiyo inamwachia Lema kwa dhamana kwa masharti atakayopewa na mahakama
hiyo.
Hata hivyo, kabla hajakamilisha
uamuzi huo akiwa katika ukurasa wa 21 kati ya kurasa 22, mawakili wa Serikali
walisema Serikali inakusudia kukata rufaa juu ya uamuzi huo.
Wakati hayo yakiendelea, jana nje
ya mahakama kuu, kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi na askari
magereza waliokuwa na silaha za moto.
No comments:
Post a Comment