Rais wa Chama cha Wanasheria
Zanzibar (ZLS ), Omar Said Shaaban amemshauri Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed
Shein asiusaini Muswada wa sheria ya mafuta na gesi uliopitishwa na wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi hivi karibuni kwa madai kuwa unavunja Katiba ya Jamhuri
ya Muungano.
Omari ameeleza msimamo huo katika
barua yake ya maneno 1,293 aliyomwandikia Dk Shein akifafanua jinsi gani
muswada huo unavunja sheria na Rais huyo anavyoingizwa kwenye mtego wa kuvunja
Katiba.
Katika barua hiyo, mwanasheria hiyo
anasema, “Mheshimiwa Rais, zipo taarifa kuwa unajiandaa kuweka saini
kwenye muswada huo uliopitishwa na Baraza la Wawakilishi ili hatimaye iwe
sheria. Naomba nikunasihi uachane na mpango huo ili kujiepusha na mtego wa
jaribio la kuvunja Katiba.”
Anasisitiza, “Kwa heshima
naomba nikueleze kuwa jaribio la Serikali yako na Baraza la Wawakilishi la
Zanzibar na hatua yako ya kuweka saini muswada huo ili uwe sheria, ni uvunjaji
mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo wewe umeapa
kuilinda, lakini pia ni kinyume na maelekezo ya sheria inayorejewa kama ndiyo
chanzo cha mamlaka ya Zanzibar kutunga sheria yake.”
Mwanasheria huyo anabainisha kuwa
kama kweli nia ya dhati ipo ya kuondoa mafuta na gesi kwenye Muungano, hatua
pekee na salama kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kusukuma kumalizika
kwa mchakato wa Katiba Mpya au kupelekwa mabadiliko ya Katiba Bungeni kuliondoa
jambo hilo kwenye Nyongeza ya Kwanza ya Katiba.
Omari alisema akiwa mwanasheria
tena kiongozi kwenye kada hiyo, ana wajibu wa kikatiba, kimamlaka na kitaaluma
kusimamia ulindwaji na usimamizi wa Katiba na sheria za nchi na akiwa mwenye
uchungu na Zanzibar, anapenda kuona ikisimamia rasilimali zake yenyewe bila ya
kukiuka masharti ya Katiba.
Alibainisha kuwa katika Katiba ya
Muungano kwenye nyongeza ya kwanza, suala la mafuta na gesi ni jambo la
Muungano hivyo usimamizi wake na utungiwaji sheria kwa mujibu wa Katiba zote
mbili upo chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment