Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Elimu,
Joseph Mungai unatarajiwa kuagwa Dar es Salaam leo katika viwanja
vya Karimjee.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, mtoto wa marehemu, William Mungai alisema ibada ya kuuaga mwili huo
itafanyika katika viwanja hivyo saa 5.00 asubuhi.
Hata hivyo mtoto huyo wa marehemu
hakutaka kuingia kwa undani kuhusu chanzo cha kifo cha baba yake, badala yake
alisema familia iachwe iendelee kushauriana na daktari.
Alisema pamoja na hayo, kifo hicho
kimewashtua kwa vile kimetokea ghafla na kwamba baada ya kuisha kwa ibada
ya kuaga mwili huo, utasafirishwa hadi Mafinga, Wilaya ya Mufindi, mkoani
Iringa kwa mazishi.
“Hadi sasa familia tunajua kwamba
marehemu aliugua tumbo la kawaida na tulimpeleka hospitalini ambako alifariki
dunia, tunaomba familia iachwe, kwa sababu bado tunashauriana na daktari
wake.
“Tumekubaliana mwili wake uagwe
kesho (leo) saa tano Viwanja vya Karimjee ambako pia historia yake yote na
familia itasomwa,” alisema William.
Kifo cha Mungai kilitokea juzi
jioni katika kile kilichoelezwa kuwa alianza kujisikia vibaya baada
ya kunywa kiywaji katika hoteli moja iliyopo Msasani, ambayo
aliizoea.
Mmoja wa waombelezaji waliofika
nyumbani kwa marehemu jana ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema)- Zanzibar, Salum Mwalimu ambaye alimwelezea
Mungai kuwa aliunga mkono mabadiliko ya siasa.
“Hakuwa na kadi ya Chadema lakini
alipenda mabadiliko, mwanaye William aligombea ubunge wa Mafinga kupitia
Chadema na baba yake alimuunga mkono,” alisema.
Mbunge wa zamani wa Kwela, Chrisant
Mzindakaya alisema amesikitishwa na kifo hicho ikizingatiwa wiki iliyopita
walikuwa pamoja na walizungumza mambo mengi ya siasa.
“Hakuwa na kesho katika maisha
yake, alilokuwa na uwezo wa kulifanya alilifanya siku hiyo hiyo, alikuwa na
msimamo, hakukubali kuyumbishwa,” alisema Mzindakaya.
Wakati huohuo, mwili wa aliyekuwa
Spika wa Bunge, Samuel Sitta unatarajiwa kuwasili leo ukitokea Ujerumani
ambako alikuwa akitibiwa hadi mauti yalipomfika.
Taarifa zilizotolewa na msemaji wa
familia ya marehemu, Gerald Mongella, zinasema mwili huo utawasili katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 9.00 mchana na kupelekwa
nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam.
“Ijumaa(kesho) saa tatu asubuhi
ibada ya kuuaga mwili huo itafanyika katika viwanja vya Karimjee ambako ndugu
na wakazi wa Dar es Salaam watapata fursa ya kuaga,” alisema Mongella.
Mwili wa Sitta utasafirishwa hadi
Dodoma ambako utaagwa na wabunge na baadaye utasafirishwa kwenda Urambo kwa
mazishi Jumamosi.
Sitta alifariki Novemba 07 mwaka
huu katika Hospitali ya Technal University alipokuwa akipatiwa matibabu ya
maradhi ya saratani ya tezi dume.
No comments:
Post a Comment