Ushabiki ni mzuri kufurahia, ni mzuri kupongezana, lakini pale
unapoingiza matusi, hakika matokeo yake ni mabaya siku zote.
Ama
pengine ushabiki kimuziki tulionao Tanzania, ubaki kuwa wa kurushiana matusi tu
ndani kwa ndani na usihusishe wasanii wa nje ambao timu zetu hazihusiani nao
asilani.
Ninasikitishwa sana na ninachokiona
kwenye ukurasa wa Instagram wa Wizkid baada ya kubainika kuwa tuzo ya MTV EMA
aliyokuwa ameshinda awali itachukuliwa na atapewa Alikiba – ambaye kwa mujibu
wa kura ndiye aliyestahili kushinda. Hiyo imekuwa habari njema kwa mashabiki wa
Alikiba. Wanastahili kufurahia – actually, Watanzania wote bila kujali timu
zilizopo tunapaswa kufurahia na kumpongeza Kiba kwa hatimaye kututoa
kimasomaso.
Lakini kwanini Wizkid ambaye naye
alipewa tu tuzo hiyo (si kama aliwawekea MTV EMA mtutu wa bunduki ili wampe)
atukanwe? Kwanini mashabiki wanataka kutengeneza uadui si tu kati ya Wizkid na
Alikiba, bali ni Nigeria na Tanzania?
Unadhani mashabiki wa Wizkid au
Wanaijeria kwa ujumla wanapenda kuona msanii wao anatukanwa bila sababu?
Kwanini hatuwezi tu kufurahia ushindi huu bila kumtusi, kumkejeli Wizkid ambaye
kwa miaka yote amekuwa akiipenda sana nchi yetu? Isitoshe Alikiba amempongeza
Wizkid kwa ushindi wake.
Sasa kwanini mashabiki wanashindwa
kutambua kuwa msanii wanayempenda anahitaji kushirikiana na wasanii hawa na sio
kutengenezewa tension baina yao isiyokuwa na faida! Nigeria ni sehemu muhimu
Afrika kimuziki, si jambo la heri kwa msanii wa Tanzania kukimwagia mchanga
kitumbua anachoweza kuhitaji kutoka huko siku za usoni.
Anachofanyiwa Wiz kwenye ukurasa wake ni aibu
inayoirudia Tanzania. Watu wachache wanaharibu jina la nchi kwa kuendekeza
ushabiki usiokuwa na afya. Na pengine ndio maana Wiz ametweet: Too many dumb people in the world. God help us!
Ombi kwa baadhi ya mashabiki wa
Alikiba ama tu wengine ambao wameamua kutumia nafasi hiyo kumharibia siku
Wizkid: Tunajidhalilisha kwa tunachokifanya. Hakuna faida ya maneno
tunayomwandikia msanii huyu kipenzi cha wengi Afrika na duniani kwa ujumla.
Tufurahi kuwa tuzo inakuja Tanzania na tumpongeze Ali kwa ushindi huo, basi!
No comments:
Post a Comment