Jumla ya wanafunzi hewa 65,198 wamegundulika kuwepo katika shule za
msingi na sekondari nchini, ambako idadi ya wanafunzi hao isingebainika kiasi
cha Sh milioni 931.3 zingepelekwa shuleni kuhudumia wanafunzi hewa kwa mwaka wa
fedha 2016/2017.
Katika
mkutano na waandishi wa habari jana mjini hapa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alisema
kati ya wanafunzi hao wa shule za msingi ni 52,783 na sekondari ni 12,415.
Simbachawene alisema kazi ya
uhakiki wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari ilifanyika mikoa yote
nchini kutokana na agizo la Ofisi ya Rais, Tamisemi kwa makatibu tawala wa
mikoa yote ya Tanzania Bara.
Alisema waliagizwa kuhakiki idadi
ya wanafunzi katika shule zote za msingi na sekondari kwa kulinganisha taarifa
ilivyokuwa Machi mwaka huu wakati wa ujazaji wa madodoso ya takwimu za shule za
awali, takwimu za shule za msingi, sekondari na nyaraka za mahudhurio ya
wanafunzi.
Alieleza kuwa taarifa za idadi ya
wanafunzi kabla ya kuhakiki Machi 2016, zilionesha kulikuwa na wanafunzi
9,746,534 wa shule za msingi na wanafunzi 1,483,872 wa shule za sekondari.
“Baada ya uhakiki tuliofanya
Septemba mwaka huu, inaonesha kuwepo wanafunzi 9,690,038 wa shule za msingi na
wanafunzi 1,429,314 wa shule za sekondari,” alieleza na kuongeza kuwa uchambuzi
umeonesha kuwa wanafunzi 52,783 wa shule za msingi na wanafunzi 12,415 wa
sekondari hawakutolewa maelezo ya uwepo wao shuleni.
Alisema kwa tafsiri rahisi hao ni
wanafunzi hewa kwa shule za msingi na sekondari nchini, ambao idadi hiyo ya
wanafunzi hewa kama isingebainika kwenye uhakiki huo na kupelekwa fedha, Sh
milioni 931.3 zingepelekwa shuleni kuhudumia wanafunzi hewa katika mwaka wa
fedha 2016/2017.
Alisema kati ya fedha hizo Sh
milioni 527.8 ni kwa shule za msingi na Sh milioni 403.4 ni kwa shule za
sekondari.
Aliitaja mikoa inayoongoza kuwa na
wanafunzi hewa ni Tabora (12,112), Ruvuma (7,743), Mwanza (7,349), Dar es
Salaam (4,096), Kagera (4,763), Rukwa (4,054), Singida (3,239), Kilimanjaro
(2,594), Kigoma (2,323), Njombe (2,307), Simiyu (2,081) na Arusha (1,923).
Mikoa mingine ni Mara (1,855),
Tanga (1,378), Geita (1,281), Morogoro (1,172), Mtwara (882), Mbeya (786),
Shinyanga (695), Songwe (512), Manyara (330), Dodoma (284), Lindi (281), Pwani
(187), Iringa (161) na Katavi (0).
Waziri huyo alisema wanafunzi hewa
walianza wakati serikali ilipoanza kupeleka fedha shuleni kama ruzuku.
No comments:
Post a Comment