Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya
ya Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP),Christopher Bageni amewasilisha
maombi Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kupinga adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
SP Bageni alihukumiwa adhabu hiyo
baada ya mahakama hiyo kujiridhisha kwamba aliwaua kwa kukusudia
wafanyabiashara wanne wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva teksi
mkazi wa Manzese, Dar es Salaam, katika Msitu wa Pande.
Bageni kupitia Wakili wake, Gaudioz
Ishengoma, aliwasilisha maombi hayo mwishoni mwa wiki yaliyoambatana na
hati ya kiapo iliyoapwa na wakili huyo.
Muwasilisha maombi anaomba mahakama
hiyo kuifanyia marejeo hukumu dhidi yake iliyotolewa Septemba 13 na
kusomwa Septemba 16 mwaka huu na Msajili wa Mahakama hiyo, John Kahyoza.
Akitoa sababu kuomba marejeo,
anadai alinyimwa haki sawa ya kusikilizwa wakati wa kutathmini ushahidi
ulioko kwenye kumbukumbu za mahakama kwa kuegemea kwenye ushahidi wa upande wa
mashtaka.
Alidai katika kuchanganua ushahidi
ambao uamuzi wa mahakama uliegemea, mahakama ilishughulika na ushahidi wa
msingi (Exam in Chief) wa upande wa mashtaka na iliangalia kwa juu juu tu
ushahidi wa utetezi hususan wa Bageni au haikuutazama kabisa.
“Kuna kukinzana kwa haki kwa maana
ya kwamba mtoa maombi alinyimwa haki sawa ya kusikilizwa, kwa mahakama kuchagua
na kuegemea upande wa mashtaka pekee na kushindwa kuzingatia
ushahidi wa upande wa utetezi, hasa wa mtoa maombi.
“Uamuzi wa mahakama umetolewa
katika msingi wa makosa ya dhahiri kwenye kumbukumbu za mahakama, hivyo
kusababisha upotoshaji wa haki, kushindwa kuzingatia mwongozo wa kanuni katika
asili, thamani na matumizi ya ushahidi wa kuungwa mkono,” ilisema sehemu ya
maombi hayo.
Alidai kuwa kwa kushindwa
kuchanganua na kutathmini ushahidi kwa umakini kwenye kumbukumbu,
mahakama ilishindwa kuainisha ushahidi wa mjibu rufaa wa nne (Bageni)
kimazingira kama ilivyo ni dhahiri unakosa thamani ya kuhitaji ushahidi wa
kuunga mkono na hivyo si salama kuegemea katika kumtia hatiani.
“Kwa kushindwa kuona na kuzingatia
ushahidi uliokusudiwa kuwa na ushahidi wa kuunga mkono, siyo ushahidi huru na
hauna mashiko kuthibitishwa (PW27) na haupo (PW36).
“Kwa kushindwa kufanya uchambuzi wa
ushahidi kwenye kumbukumbu kwa umakini wenye manufaa, vinginevyo mahakama
ilipaswa kuona wajibu wa kuthibitisha shtaka kwenye jinai haukufikiwa,”anasema Wakili
Ishengoma.
Anadai mahakama katika kuamua, kama
ilivyofanya katika uhalisia wake, kuhusu ushiriki wa mtoa maombi katika eneo la
tukio la uhalifu, ilishindwa kubaini katika ujumla wake ushahidi wa upande wa
mashtaka ambao haukuweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.
Ishengoma alidai mahakama
haikuuchukulia ushahidi kwenye kumbukumbu katika ujumla wake hivyo kutengua uamuzi
wa kuachiwa huru kwa mtoa maombi na kumtia hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifo
kwa kusimamia ushahidi ambao haupo na uvumi pamoja na ushahidi wa mashaka
makubwa.
Alidai kutokana na hukumu ya
mahakama, haikuwa bayana ni kwa ushahidi wa nani ulithibisha mtoa maombi Bageni
alimwezesha au kumsaidia nani katika mauaji ya marehemu hao.
Katika hati ya kiapo iliyoapwa na
Wakili Ishengoma, Bageni anadai yeye na wengine wanane ambao hawako katika
maombi hayo walishtakiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa makosa ya
mauaji ya watu wanne katika Kesi ya jinai namba 26 ya mwaka 2006.
Bageni alikuwa mshtakiwa wa pili na
katika hukumu iliyotolewa na Jaji Salum Massati, amnayo wote waliachiwa
huru, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hakuridhishwa na uamuzi huo hivyo
alikata rufaa namba 358 ya mwaka 2013.
Kabla ya usikilizwaji wa rufaa
hiyo, DPP aliwaondolea rufaa wajibu rufaa watano na kubaki wajibu rufani wanne
ambao waliachiwa huru pia Septemba 16, mwaka huu.
Walioachiwa huru ni aliyekuwa Mkuu
wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah
Zombe na maofisa wengine wawili baada ya mahakama kuona hakuna ushahidi wa wazi
ama mazingira kuwatia hatiani.
Katika kesi ya msingi, Bageni
alidaiwa kuwaua kwa kukusudia wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, maarufu Jongo
na ndugu yake, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, aliyekuwa
dereva wa teksi wa Manzese , Januari 14, mwaka 2006, katika Msitu wa Pande,
Mbezi Luis, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment