Taasisi ya The Desk &
Chair Foundation (TD& CF), inatarajia kujenga vyoo 100 katika Barabara Kuu
ya Mwanza-Shinyanga-Dar es Salaam unaokadiriwa kutumia Sh. milioni 500.
Mwenyekiti wa TD & CF, Alhaji
Sibtain Meghjee alisema hivi karibuni mjini Mwanza kwamba mradi huo ni sehemu
ya miradi mitatu mikubwa ambayo taasisi yake inatekeleza nchini.
Alisema baada ya kukamilisha mradi
mkubwa wa jengo la kupumzikia wananchi wanaokwenda kutibiwa na kuwajulia
hali wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou
Toure wanatarajia kujenga vyoo 100 kwenye barabara ya kutoka Mwanza hadi
Dar es Salaam kwa basi.
Meghjee alieleza kuwa maandalizi ya
awali ya mradi huo yameshaanza na kwamba watashirikiana na Mamlaka ya Udhibiti
wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) na Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS) ili kupata taarifa sahihi kabla ya mradi kuanza.
“Penye nia pana njia, baada ya
kukamilisha ndoto yetu, leo ya mradi huu mkubwa wa ujenzi wa jengo la
kupumzikia hapa Sekou Toure, tunatarajiwa kutekeleza miradi mitatu mikubwa
ukiwemo wa vyoo kwa ajili ya abiria wanaosafiri kati ya Mwanza na Dar es
Salaam:
“Tunataka msamiati wa kuchimba dawa
wakati wa safari ubaki kuwa historia kwa hiyo tunatarajia kufanya jaribio moja
la kujenga matundu 100 ya vyoo katika njia na barabara kuu ya Mwanza hadi Dar
es salaam ambavyo vitagharimu shilingi milioni 500.Tutashirikiana na mamlaka
husika, ofisi yako na idara ya afya,”alisema Meghjee.
Meghjee alieleza kuwa taasisi hiyo
pia ina mpango wa kutekeleza mradi wa kutengeneza viungo bandia kwa
kushirikiana na kitengo cha Jairpur Foot/Knee and Limb Project cha India ambao
unahitaji Dola 200,000 za Marekani (sh. milioni 44), zitakazowezesha kuanzisha
huduma ya viungo hivyo bandia vya miguu, mikono, fimbo na baiskeli.
Alisema wanaendelea kuwasiliana na
wafadhili watakaoshirikiana nao kwenye mradi huo na kuwahakikishia walengwa kuwa
viungo hivyo vitapatikana kwa gharama nafuu mara utakapokamilika mradi huo.
Meghjee aliongeza kuwa wakati
wakiendesha ujenzi wa jengo la mapumziko katika Hospitali ya Sekou
Toure,walipata wazo la kujenga mabanda yatakayotumiwa na madereva wa pikipiki (boda
boda) kuegesha vyombo vyao kivulini na kupata huduma ya vyoo na mabafu.
Mwenyekiti huyo wa TD & CF
aliongeza zaidi kuwa endapo Halmashauri ya Jiji itaridhia na kuwapa eneo
maalumu na mahususi la ujenzi wa huduma hiyo watafanya jaribio hilo moja ili kuweza
kuona matunda yake.
No comments:
Post a Comment