Mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema ameendelea kusota katika mahabusu ya Gereza la Kisongo mjini
Arusha akiingiza siku ya 22 leo baada ya jana kukwama katika azma yake ya
kutaka Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kufanya marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Arusha uliomnyima dhamana.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu
Kanda ya Arusha, Sekela Moshi ndiye aliyetupilia mbali ombi la Lema, hivyo
kumfanya arejee mahabusu huku mawakili wake wakihaha kuhakikisha wanakata rufaa
ili kuomba dhamana hiyo katika ngazi nyingine ya kisheria.
Aidha, Jaji Moshi ameridhia ombi la
Lema kupitia kwa mawakili wake Sheck Mfinanga na Peter Kibatala la kukata rufaa
mahakamani hapo ili kesi hiyo isikilizwe na hatimaye Lema kupata dhamana baada
ya kupitiwa na jaji atakayepangiwa.
Akitoa uamuzi huo mahakamani hapo,
Jaji Moshi alisema kimsingi hoja ya mawakili wa Lema ya kutaka mahakama hiyo
kuitisha faili na kulipitia haina msingi wowote kisheria hivyo anaitupilia
mbali hoja hiyo na kutoa rai kwa mawakili hao kukata rufaa Mahakama ya Rufaa
ili dhamana ya Lema isikilizwe.
“Mahakama hii haiwezi kupitia faili
la kesi hii ya Lema ya kupata dhamana hivyo siwezi kupitia faili hili, bali
nashauri mkate rufaa ili iweze kusikilizwa,” alisema Jaji Moshi.
Awali Wakili wa Serikali, Paul
Kadushi aliwasilisha pingamizi Mahakama Kuu la kuitaka wasisikilize maombi ya
Lema ya kutaka mahakama hiyo iitishe faili la kesi namba 440/441 kwa madai yapo
makosa ya kisheria yaliyofanywa awali na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa
lengo la kumnyima dhamana mbunge huyo.
Akiwasilisha hoja zake mbele ya
Jaji Moshi katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Kadushi akisaidiana na Materu
Marandu alisema anawasilisha hoja mbili za pingamizi za mahakama hiyo kuendelea
kusikiliza kesi hiyo.
Alisema kimsingi maombi hayo
yaliwasilishwa mahakamani hapo kutaka mahakama hiyo iitishe faili la kesi namba
440/441 yanakinzana na kifungu cha 43 (2) cha sheria ya Mahakama ya Mahakimu.
Katika kesi hiyo, Lema anashitakiwa kwa kutoa maneno ya kumtusi Rais katika
maeneo tofauti.
Kadushi alisema uamuzi unaopinga
kufanywa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ya kukubali kutompa dhamana Lema ni
uamuzi mdogo na haukuwa na sababu za kukataa dhamana.
“Mahakama yako inafungwa mikono na
kifungu hiki kufanya mapitio au uamuzi mdogo, hivyo tunaomba mahakama itupilie
mbali maombi hayo,”alisema Kadushi ambaye wakati akiwasilisha hoja zake alikuwa
akinukuu mashauri mbalimbali ya kesi zinazofanana na hiyo.
Aidha, Kadushi alisisitiza kuwa wao
wanatambua haki ya kukata rufaa ipo wazi kwa mleta maombi ila itakuwa jambo
geni kama mahakama itawapa nafasi kusikiliza maombi yao.
Alisema hoja ya pili ya
pingamizi lake, linatokana na mleta maombi kutokidhi matakwa ya kisheria ya
mwenendo wa makosa ya jinai.
Katika sheria ya makosa ya jinai,
kifungu cha 359(1) ya mwaka 2002 kuwa mtu asiporidhika na maamuzi ya mahakama
ya chini kama ilivyo katika kesi hiyo, kamwe hawezi kuwa na mbadala wa mapitio
ya rufaa.
Akijibu hoja hizo Wakili
anayemtetea Lema, Peter Kibatala akiwa na jopo la mawakili wenzake, Adam Jabir,
Sheck Mfinanga, John Mallya, Faraji Mangula na Charles Adiel, alipinga kuwekewa
pingamizi hilo na kuomba mahakama isikilize maombi yao.
Alisema wao wamefungua maombi hayo
kuiomba Mahakama Kuu kuitisha jalada la kesi ya mahakama ya chini ili kuona
uhalali wa kutotekelezwa kwa uamuzi wa kutoa dhamana, kwani kilichokuwa
kinasubiriwa ni masharti ya dhamana.
“Huyu mshitakiwa alipewa dhamana ,
ila kabla ya mahakama haijatoa masharti ya dhamana, upande wa serikali
ukasimama kabla mahakama haijaweka masharti ya dhamana ambayo lazima ifanye
hivyo, wakasema wameonesha nia ya kukata rufaa na mahakama ikakubaliana nao
bila kutekeleza amri yao,” alisema Kibatala.
Aliomba mahakama hiyo itupilie
mbali pingamizi la serikali na kuiomba kuendelea na kazi iliyokusudia kuifanya
ya kupitia maombi yao ili kutoa dhamana kwa mshtakiwa au iamuru mahakama ya
chini kuendelea na uamuzi wake.
Wakili wa mbunge huyo baada ya
maombi yao kugonga mwamba, walikuwa kwenye hekaheka ya kukamilisha kuandika
rufaa ili kumnasua Lema atoke mahabusu.
Baada ya kutoka nje ya Mahakama
Kuu, Wakili Mfinanga alisema wanamalizia kukamilisha taratibu za wao kukata
rufaa Mahakama Kuu na wataomba rufaa hiyo isikilizwe kwa hati ya dharura ili
kumnasua Lema mahabusu.
No comments:
Post a Comment