Mahakama ya Mafisadi yaendelea kupiga kazi....Yatupilia Mbali Pingamizi la DPP Dhidi ya Watanzania na Mchina Mmoja - OREST NGOWI

Breaking

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Tuesday, 15 November 2016

Mahakama ya Mafisadi yaendelea kupiga kazi....Yatupilia Mbali Pingamizi la DPP Dhidi ya Watanzania na Mchina Mmoja

   
Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Ufisadi imetupilia mbali pingamizi lililowekwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuhusu mamlaka iliyonayo katika kutoa dhamana kwa washtakiwa wa makosa ya rushwa.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo Rehema Mkuye aliyesikiliza pingamizi la DPP dhidi ya maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na washtakiwa wawili wa kesi ya Uhujumu Uchumi, wanaokabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Washtakiwa hao ni Mtanzania, Jeremiah Madar Kerenge (40) pamoja na Fu Chang Feng (50), raia wa China, na Ally Damji Raza (34) raia wa India, ambao wanadaiwa kukutwa na nyavu haramu za kuvulia samaki zenye thamani ya jumla ya Sh22, 978,750,000.

Kerenge na Raza waliwasilisha maombi ya dhamana katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, lakini DPP aliweka pingamizi akidai maombi hayo yamefunguliwa kwenye mahakama isiyo sahihi. 

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo Novemba 3, DPP kupitia kwa Wakili wa Serikali Mkuu (PSA) Vitalis Timon alifafanua kuwa sheria inataka maombi hayo yafunguliwe Mahakama Kuu na siyo katika Mahakama ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Hata hivyo, katika uamuzi wake jana, mahakama hiyo ilitupilia mbali pingamizi hilo la DPP na ikasema kuwa ina uwezo na kwamba mahakamani hapo ndipo mahali sahihi pa kufungua maombi ya dhamana kwa washtakiwa wote wa kesi za rushwa na uhujumu uchumi.

Kuhusu kifungu cha 29 (4) (d) cha Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi kinachoonyesha kuwa Mahakama Kuu ya kawaida ndio yenye mamlaka ya kutoa dhamana kwa washtakiwa wa rushwa au uhujumu uchumi, Jaji Mkuye alisema kuwa kuna makosa.

Alifafanua kuwa kinachoonekana katika kifungu hicho ni usahaulifu tu wa Bunge na kwamba nacho kilipaswa kufanyiwa marekebisho, kitamke kuwa maombi ya dhamana katika kesi ya rushwa na uhujumu uchumi, lazima yafunguliwe katika Divesheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Alisema kuwa kwa kuwa divisheni hiyo ina ofisi katika kila Kanda ya Mahakama Kuu, ambako pia tayari kuna majaji maalumu walioteuliwa kushughulikia kesi na maombi ya dhamana ya kesi za rushwa na uhujumu uchumi, hivyo hakuna hofu yoyote ya mlundikano wa wananchi kusubiria maombi yao.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo Novemba 3, Wakili Vitalis alidai kuwa mahakama hiyo inakuwa na uwezo wa kutoa dhamana pale tu ambapo kesi ya msingi inakuwa tayari imeshafunguliwa kwenye mahakama hiyo.

Hata hivyo, wakili wa washtakiwa hao, Roman Lamwai alipinga hoja hizo akidai kuwa mahakama hiyo ndio mahali sahihi kwa mujibu wa tafsri ya Sheria ya Uhujumu Uchumi kama ilivyofanyiwa marekebisho.

Alisisitiza kuwa hata ukubwa wa kiwango cha pesa katika hati ya mashtaka kwenye kesi hiyo ni lazima maombi hayo yafunguliwe katika mahakama hiyo ambavyo ndio yenye jukumu la kusikiliza na kuamua kesi za Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Baada ya Mahakama kutupilia mbali pingamizi hilo, iliendelea kusikiliza maombi ya dhamana ambapo Wakili Lamwai aliieleza mahakama kuwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao yanadhaminika na kwamba wote wako tayari kutekeleza masharti ya dhamana.

Lamwai alidai kuwa mtoa maombi wa kwanza (Kerenge) ana mke ambaye ni mjamzito hivyo anahitaji kuwa naye karibu kumhudumia. 

Kuhusu mtoa maombi wa pili (Raza), alidai kuwa mashtaka mawili yote yanayomkabili hayaangukii kwenye sheria ya Uhujumu uchumi, lakini kwa kuwa yameambatanishwa kwenye kesi ya uhujumu uchumi basi dhamana yake ilikuwa vigumu katika mahakama ya chini.

Aliongeza kuwa yeye ni mfanyabiashara anayefanya biashara zake Dar es Salaam ambako pia ndiko aliko na makazi yake ya kudumu hivyo hawezi kuruka dhamana.

Akijibu hoja za maombi hayo, Wakili Timon alidai kuwa baada ya pingamizi lao kutupiliwa mbali, hawana pingamizi kuhusu dhamana, kwa kuwa mashtaka yanayowakabili yanadhaminika na pia dhamana ni haki yao.

Hata hivyo aliikumbusha mahakama kuwa wakati wa kutoa dhamana izingatie kifungu cha 36 (5) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2016.

Kwamba kwa mujibu wa kifungu hicho, watoa maombi wanalazimika kuwasilisha mahakamani pesa taslimu au hati ya mali yenye thamani sawa na nusu ya pesa inayotajwa kwenye hati ya mashtaka, kwa utaratibu wa kanuni ya kugawana au kuchangia wote kiwango hicho cha pesa.


Baada ya kusikiliza hoja za kila upande, Jaji Mkuye aliahirisha shauri hilo hadi kesho atakapotoa uamuzi wa dhamana kwa washtakiwa hao. 

Katika kesi ya msingi namba 45 ya mwaka 2016, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa wa Mahakama ya Kisutu, inadaiwa walikutwa na nyavu ambazo zimepigwa marufuku kutumika wala kuhifadhiwa nchini zenye thamani ya jumla ya Sh22, 978,750,000.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here