Mfanyakazi wa ndani wa Mbunge wa
Bunge la Afrika Mashariki, Angella Kizigha, Miraji Mkanga (41) amepandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam kwa madai ya
kumwibia mwajiri wake vitu ikiwemo bastola yenye risasi 23, simu, mikufu na
bangili za dhahabu, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 85.
Akisomewa mashitaka hayo na Karani
Dayz Makalala mbele ya Hakimu Joyce Mushi, ilidaiwa kuwa mshitakiwa Mkanga
alitenda kosa hilo Oktoba 2, mwaka huu maeneo ya Kijitonyama wilaya ya
Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Makakala alidai mtuhumiwa huyo
aliiba Dola za Marekani 3,500 zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 7.5, bangili
za dhahabu gramu 300 zenye thamani ya Sh milioni 36, hereni gramu 450 zenye
thamani ya Sh milioni 42, doti 30 za vitenge zenye thamani ya Sh milioni 1.5 na
shuka 10 zenye thamani ya Sh 700,000.
Aidha, mfanyakazi huyo wa ndani
anatuhumiwa kuiba bastola moja iliyotengenezwa Jamhuri ya Czech yenye namba No
B 283994 na risasi 23 thamani ya Sh milioni mbili, simu mbili za Samsung zenye
thamani ya Sh 500,000 na nguo tofauti zenye thamani ya Sh 750,000 mali ya
mbunge huyo ambaye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mshitakiwa alikana shitaka hilo
wakati huo dhamana yake ipo wazi, akitakiwa kuwa na wadhamini wawili kutoka
katika taasisi inayotambulika na kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni tano
kila mmoja.
Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena
Novemba 28, mwaka huu, na mshitakiwa alirudishwa rumande kutokana na wadhamini
wake kutofika huku upelelezi ukiendelea.
No comments:
Post a Comment