Katika kuendelea kujenga
dhana ya kubana matumizi ya fedha za serikali, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
amesafiri kwa ndege ya abiria ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Dar es
Salaam kwenda Mwanza na kuokoa zaidi ya Sh milioni 33.
Kabla ya kuanza safari hiyo jana kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais
akizungumza na waandishi wa habari, alisema kwa kupanda ndege hiyo ameokoa
fedha za serikali na kodi za wananchi.
Alisema ameona ashirikiane na
Watanzania kuonesha uzalendo kwa kutumia huduma ambazo zinatolewa na serikali
na kuwataka Watanzania wote kutumia ndege hizo.
“Ningepanda ndege ya kukodi
ningetumia shilingi milioni 40 kwa safari hii, lakini nikaona hapana nikaamua
mimi pamoja na msafara wangu tutumie ndege hii ya Shirika la Ndege Tanzania
ambapo tumetumia Shilingi milioni 7.6 pekee,” alisema Makamu wa
Rais aliyeambatana na watu 16 katika safari hiyo.
Makamu wa Rais ambaye alipanda
ndege hiyo pamoja na abiria wengine wa kawaida, aliwataka viongozi wengine pia
kufuata mfano huo kusafiri kwa kutumia ndege za shirika hilo.
Alisema ameona kwenye televisheni
watu wakitoa maoni yao juu ya kampuni hiyo ya ndege kuwa ni nzuri kwa sasa na
yeye akaamua kusafiri na ndege hiyo.
“Niliona kwenye televisheni watu
wakitoa maoni mazuri tu juu ya shirika hili na mimi nikaona nitumie nafasi
hiyo,” alifafanua Makamu wa Rais.
Hivi karibuni, serikali imenunua
ndege mbili aina ya Bombardier Q400 na kuzikabidhiwa kwa ATCL na zimeanza
kufanya kazi katika mikoa mbalimbali nchini huku zikiwa na gharama nafuu,
lakini pia zikiwa na gharama nafuu ya uendeshaji.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ambaye alikuwepo uwanjani akimsindikiza
Makamu wa Rais, alisema Watanzania waelewe kwa sasa kampuni hiyo iko kwa ajili
ya kufanya biashara.
Alimpongeza Makamu wa Rais kwa
kuonesha ushirikiano mkubwa na pia uzalendo kwa kusafiri na ndege ya ATCL,
kwani angeweza kutumia ndege nyingine yoyote.
“Leo hii kwa kutumia ndege ya
Tanzania yeye pamoja na wasaidizi wake ni jambo jema sana alilolifanya na pia
ni jambo la kizalendo tunampongeza sana, kwani angeweza kutumia ndege nyingine
yoyote anayoitaka,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema ndege za ATCL gharama zake
ni nafuu na pia huduma zao zimeboreshwa zaidi, na kwamba ifikapo mwaka 2018
serikali itanunua ndege nyingine moja na pia mwaka 2019 inatarajia kununua
ndege nyingine.
Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus
Matindi alisema kampuni hiyo inaboresha huduma zake ambako kwa sasa wanaboresha
huduma za mtandaoni kwa ajili ya watu kushika nafasi ya safari na hata kulipia
kupitia mitandao ya simu.
No comments:
Post a Comment