Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
amesema atamwajibisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda iwapo
hatasimamia ipasavyo kukomesha matumizi ya dawa za kulevya, aina ya shisha.
Hatua hiyo inatokana na kauli ya
Makonda kuwatuhumu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna
wa Polisi Simon Sirro na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi
Suzan Kaganda, kulegalega kusimamia suala hilo huku akihofia wanaweza kuwa
wamehongwa na watu waliotaka kumhonga lakini akakataa.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema hayo
jana wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Umeme katika
Jiji la Dar es Salaam.
Alisema katika udhibiti wa suala la
shisha, mkuu huyo wa mkoa amefanya kazi nzuri, na kwamba kwa kuwa ameshatoa
maelekezo, akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Makonda
hana budi kuyatekeleza.
Alisema alivyosikia anawaagiza
wakuu wake wa wilaya wote kusimamia maagizo yake na kama hawakusimamia
atachukua hatua, basi naye atachukua hatua kwake (Makonda) asipotekeleza suala
hilo ambalo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni tatizo kubwa.
“Sasa mimi nasema nakuagiza wewe
usimamie na kama hutasimamia suala hilo nitakuchukulia hatua, hivyo hangaika na
shisha kwa wanaopuliza wakiwa wamelala hakikisha unawadhibiti,” alisema Waziri
Mkuu Majaliwa wakati akijibu sehemu ya salamu za Makonda alipopewa fursa ya
kusalimia wananchi katika hafla hiyo.
Katika salamu zake, Makonda alisema
Waziri Mkuu alipiga marufuku matumizi ya shisha, hivyo alimwagiza Kamanda Sirro
kuhakikisha suala hilo linatekelezwa kwa kiwango kikubwa.
“Lakini Waziri Mkuu nimeshangaa
kupita katika baadhi ya maeneo na kuona watu wameanza tena kuvuta shisha na
nilipouliza wakasema wewe ndiyo umetoa kibali cha shisha,” alieleza Makonda
na kuongeza alishangaa Waziri Mkuu alipiga marufuku shisha, ni lini ametoa
kibali kuanza kutumika.
Lakini mkuu huyo wa mkoa alienda
mbali zaidi na kudai kuna kikundi cha watu 10 waliokwenda kwake ambao
anawatambua kama “maajenti wa shetani” ambao wanapata faida kati ya Sh milioni
35 mpaka Sh milioni 45 kwa mwezi kutokana na dawa hizo za kulevya.
Alidai watu hao walipanga mikakati
ya kumshawishi kupokea Sh milioni tano kwa kila mmoja kwa mwezi yaani Sh
milioni 50 ili asipige kelele kuhusu shisha na wao waendelee kupata
faida.
“Shisha imerudi katika Mkoa wa Dar
es Salaam na nimeshamuagiza Kamishna Sirro, lakini nimeona kama ana kigugumizi…
lakini sijajua kama hizi tano tano zimepita kwake na pia RPC wa Kinondoni
nimemuona hapa, lakini hawa wana kigugumizi sijui kama hizi tano tano zimepita
kwao,” alisema Makonda.
Alisema aliamua kufanya ziara
mwenyewe na kushuhudia watoto wadogo wanavuta shisha, hivyo uwezekano miaka 10
ijayo vijana wengi kuwa matatizo ya afya, hivyo kumwomba Waziri Mkuu kutochoka
kusimamia suala hilo na taasisi zote ili likome katika mikoa yote.
Kuhusu wafanyabiashara wadogo,
alisema suala hilo linamnyima usingizi na kutoa rai kwa wakuu wa wilaya kuwa,
kama kuna mkuu wa wilaya atachelewa kutekeleza yale aliyoagiza kuwapeleka
machinga katika maeneo yaliyoruhusiwa atachukua hatua kabla ya Waziri Mkuu
kufanya hivyo.
Aidha, alishukuru kwa mradi wa
umeme akisema ukatikaji umeme una madhara sana na hasa kwa wajasiriamali wadogo
wanaojishughulisha na biashara ndogo kama saluni na shughuli nyingine ndogo
zinazojenga uchumi wa kati.
No comments:
Post a Comment