Mawakili wa Mbunge wa Jimbo la
Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ambaye yupo mahabusu katika Gereza kuu la
Kisongo, jana walishindwa kukamilisha taratibu za kisheria za kuwasilisha
maombi ya dhamana Mahakama Kuu .
Wakili wa Lema, John Mallya jana
alisema watawasilisha maombi hayo leo wakati wa kusikilizwa kesi nyingine za
mteja wao. “Bado kuna taratibu zinaendelea na tunatarajia kesho (leo)
tutazikamilisha,” alisema Mallya.
Katibu wa Mbunge Lema, Innocent
Kisayegi, alisema baadhi ya mawakili wa Lema walikuwa na kikao cha kisheria
kujipanga kwa kesi ya leo huku wakisubiri timu nyingine ya mawakili kutoka
makao makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam.
“Muda huu leo (jana) mawakili
wanaendelea na kikao na tuna imani leo watakuwa tayari kwa utetezi wa Lema,”
alisema.
Mawakili wa Lema ambao jana
walikutana ni James Lyatuu, Sheck Mfinanga na Charles Aidieli na wanatarajia
kuungana na mawakili wengine akiwamo Mallya.
Hata hivyo, Kisayegi aliwataka
wakazi wa Arusha wajitokeze mahakamani kusikiliza kesi inayomkabili mbunge huyo
na mkewe.
Lema anakabiliwa na mashtaka ya
kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli ambayo yanatajwa
kusababisha kukosa dhamana kutokana na rufani ya dhamana yake kuwekewa pingamizi
na wanasheria wa Serikali.
Lema na mke wake, pia wanakabiliwa
na kesi ya kutuma ujumbe wa uchochezi dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho
Gambo na shitaka jingine la kuhamasisha maandamano ya Ukuta Agosti.
No comments:
Post a Comment