Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani
Simiyu imewaachia huru viongozi na wanachama 17 wa Chadema walikokuwa
wakikabiliwa na mashitaka ya kujaribu kushawishi kutenda kosa Agosti 25 katika
ofisi ya wilaya ya chama hicho Mnadani mjini hapa.
Wanachama waliachwa jana na Hakimu
Tumaini Marwa aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo baada ya upande wa mashitaka
chini ya Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Nassib Swedy kushindwa kukamilisha
upelelezi wa kesi hiyo huku wakitoa sababu mbalimbali.
Swedy alidai kuwa washitakiwa
hao wakiwa kwenye ofisi yao siku hiyo saa 7 mchana walipanga kufanya maandamano
na mikutano ya Ukuta, ambayo ingehatarisha amani na utulivu wilayani humo na
Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, washitakiwa hao ambao
awali walifikishwa mahakamani hapo Agosti 26 chini ya ulinzi mkali wa Polisi,
walikana mashitaka na kunyimwa dhamana, walidhaminiwa Septemba 2 baada ya
kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika ambaye
alisaini bondi ya Sh milioni tano.
Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu
Marwa alitupilia mbali maombi ya upande wa mashitaka yaliyokuwa yakiomba
ahirisho la kesi hiyo kwa mara nyingine ukidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo
haujakamilika.
Alisema amri ya mwisho aliyoitoa
ilikuwa ahirisho la Novemba 4 hivyo upande wa mashitaka umeshindwa kutekeleza
amri ya Mahakama na kwa maana hiyo, anawaacha huru washitakiwa wote chini ya
kifungu cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu cha 225 (5) sura ya
20.
“Kifungu hiki kilichowaacha huru
washitakiwa hakizuii Polisi kuwafikisha mahakamani tena washitakiwa kwa kosa
hilo, iwapo watakuwa wamekamilisha uchunguzi juu ya shauri linalowakabili,”
alisema Hakimu Marwa.
Hata hivyo, wakati uamuzi unatolewa
wakili wa washitakiwa hao, Martine Sabini aliyekuwa akiwakilisha washitakiwa
wote hakuwapo mahakamani, lakini alikuwa ameshawasilisha ombi mbele ya Mahakama
hiyo kuomba waachiwe huru kwa sababu ya upande wa mashitaka kushindwa
kukamilisha upepelezi kwa muda mwafaka.
Walioachiwa huru ni pamoja na
Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Maswa, Peter Shiyo (39), Katibu wa Chadema
wa Wilaya, Flora Msuka (31), Katibu wa Bawacha wa Wilaya, Elias Matondo (37)
na Katibu Mwenezi wa Maswa Mashariki, Waziri Peter (46).
Wengine ni Bundala Baya (30),
Edward Makoye (63), Sylvester Ngwege (60), Frank Makaranga (31), Selemani Kombe
(39) na Mapambano Jackson (37).
Pia Nkuba Magwila (40),
Ndebile Paul (27), Edgar Ngasa (32), Lucas Nkuba (39), Laurent Mahembo (36) na
Mwajuma Said (40).
Baada ya kuachwa, Shiyo aliishukuru
Mahakama kwa kutenda haki akilitaka Jeshi la Polisi kuacha kunyanyasa viongozi
wa vyama vya upinzani kwa kufanya kazi kwa hisia na matokeo yake, wanaitia aibu
Serikali kwa kushindwa kesi mahakamani.
No comments:
Post a Comment