Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia
Ackson amesema wabunge wanawake wamesikitishwa na kushindwa kwa mgombea urais
wa Marekani kwa tiketi ya Chama cha Democrat, Hillary Clinton.
Dk. Tulia alitoa kauli hiyo bungeni
mjini Dodoma jana, baada ya kutambulisha wageni mbalimbali.
Alisema walitarajia mambo yangekuwa
mazuri upande wao akiwa mama (wanawake), lakini haikuwezekana.
“Safari hii haikuwezekana, asikate
tamaa maana baada ya miaka minne mambo yanaweza kuwa mazuri zaidi kuliko
ilivyokuwa sasa. Nampa pole mama Clinton kwa kuwa safari hii haikuwezakana,” alisema Dk Tulia
huku akishangiliwa na wabunge wanawake na kuongeza:
“Nasikia kuna watu hapa wanasema
tungempeleka mheshimiwa fulani… katika maeneo yale mama Clinton angeshinda,” alisema.
Kutokana na kile kilichoonekana
kupigwa butwaa na uchaguzi huo, kabla ya kuuliza swali la nyongeza jana
asubuhi, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema), alisema ana masikitiko
makubwa kwa sababu Hillary Clinton ameshindwa uchaguzi.
“Kwa niaba ya wanawake wenzangu,
nampa pole mama Clinton kwa kushindwa uchaguzi, tumeumia sana na tumerudi
nyuma,” alisema.
Kauli hiyo ilimfanya Dk. Tulia
kumtaka aeleze amepata wapi taarifa wakati bado wabunge wanawake wana
faraja Hillary angeweza kushinda.
Hata hivyo, akijibu swali la Suzan,
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Khamis
Kigwangala, alimpa pole Hillary kwa kushindwa kwenye uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment