WATU sita akiwemo mfanyabiashara
Yusuf Yusuf (34) aliyewahi kutajwa na Rais John Magufuli kwa jina la ‘Mpemba’
kuwa ni kinara wa ujangili, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya
kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6.
Washtakiwa hao walipandishwa
kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, huku
baadhi wakiwa hawajavaa viatu, wakitembea kwa kuchechemea.
Baada ya kusomewa mashtaka, upande
wa Jamhuri ulidai unatarajia kuwapeleka washtakiwa hao katika Mahakama Kuu
Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama “Mahakama ya
Mafisadi” kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Washtakiwa hao watapelekwa katika
mahakama hiyo baada ya upande wa Jamhuri kuandaa maelezo ya mashahidi pamoja na
vielelezo ili kesi hiyo ianze kusikilizwa.
Yusuf pamoja na wenzake Charles
Mrutu (37) mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa (40) mkazi wa Mbagala
Chamazi, Jumanne Chima (30) mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo (33) dereva na Pius
Kulagwa (46) walisomewa mashtaka manne mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Thomas
Simba.
Akisoma mashtaka, Wakili wa
Serikali Paul Kadushi alidai katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na
Oktoba, mwaka huu wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara walijihusisha
na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za serikali ambazo ni
vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na
Sh milioni 392.8 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Aliendelea kudai kuwa katika shtaka
la pili kuwa, Oktoba 26, mwaka huu, washtakiwa wakiwa Mbagala Zakhem, walikutwa
na vipande 10 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 13.85 vyenye thamani ya
dola za Marekani 30,000 sawa na Sh milioni 65.4.
Katika mashtaka mengine, inadaiwa
Oktoba 27, mwaka huu, washtakiwa wakiwa Tabata Kisukuru walikutwa na vipande
vinne vya meno hayo vyenye uzito wa kilo 11.1 na thamani ya dola za Marekani
15,000 sawa na Sh milioni 32.7.
Aidha, Oktoba 29, mwaka huu walikutwa
na vipande 36 vyenye thamani ya Sh milioni 294.6 bila kuwa na kibali cha
Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Hakimu Simba alisema washtakiwa
hawatakiwi kujibu mashtaka yao kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza
kesi hiyo, hivyo aliiahirisha hadi Desemba mosi mwaka huu.
Kabla ya kutoka kwenye chumba cha
mahakama, washtakiwa walimuomba hakimu awape muda waeleze jinsi walivyokamatwa
kwa kuwa walipigwa sana. Mpemba alidai siku aliyokamatwa, alipigwa sana hadi
sasa hawezi kusikia vizuri na viungo vyake vya mwili havina nguvu hivyo aliomba
PF3 ili akatibiwe.
Mrutu alidai kuwa alipigwa hadi
wakamng’oa kidole kimoja cha mkononi na washtakiwa wengine walidai walipigwa
mpaka sasa wanashindwa kutembea vizuri hivyo waliomba wapewe msaada wa
kutibiwa.
Hakimu Simba alisema hawezi kutoa
amri ya kutolewa kwa PF3 kwa sababu Magereza wana zahanati zao na kuna taratibu
wanazifuata hivyo wasiwe na wasiwasi na kama watashindwa kuwatibia, watatafuta
utaratibu mwingine wa kuwapeleka katika hospitali za nje ya Magereza.
Baadhi ya washtakiwa, waliingia
mahakamani hapo wakiwa wanachechemea huku wakificha sura zao kukwepa kupigwa
picha. Washtakiwa wawili hawakuwa na viatu.
No comments:
Post a Comment