Wanahabari waliopewa kazi ya kufuatilia safari zake walibaki
kushangaa kwani walikuwa wameelezwa kwamba angesalia nyumbani jioni hiyo.
Lakini badala yake, aliandamana na kundi ndogo la maafisa hadi
kwenye mgawaha wa 21 Club katika mtaa wa Manhattan, mmoja wa migahawa
anayoipenda sana.
Video zilizopigwa wakati wa kisa hicho Jumatano zinamuonyesha Bw
Trump akiwasalimia wateja na kuwaambia kwamba atapunguza kodi wanayolipa kwa
serikali.
Kuwasili kwake 21 Club kulijulikana baada ya mwandishi wa
Bloomberg, Taylor Riggs, ambaye kibahati alikuwa ameenda kwenye mgahawa huo,
alipakia kwenye Twitter ujumbe wa kusema kwamba Trump alikuwa amefika kwenye
mgahawa huo. Hata hivyo, alikosea jina la eneo na badala yake akasema ilikuwa
ni Keene.
Kwneye video, Bw Trum anaonekana akiwaambia wateja:
"Tutapunguza kodi mnayolipa, msiwe na wasiwasi kuhusu hilo."
Kundi la wanahabari waliopewa kazi ya kufuatilia safari za rais
huyo mteule, inadaiwa waliambiwa na msemaji wa Bw Trump, Hope Hicks, mwendo wa
saa 18:45 kwamba alikuwa amekamilisha shughuli za siku na kwamba walikuwa huru
kwenda nyumbani.
Dakika 45 baadaye, msafara mkubwa wa magari ulionekana ukiondoka
kutoka afisi kuu ya Bw Trump kwa sasa katika jumba la Trump Tower. Msafara huo
ulijumuisha magari zaidi ya kumi na gari la kubeba wagonjwa.
Riggs alipoandika kwenye Twitter, wanahabari walikimbia mgahawa
wa Keene kabla ya kugundua kwamba alikuwa 21 Club.
Hawakuruhusiwa kuingia Trump na familia yake walipokuwa wanakula
chakula cha jioni kabla ya kiongozi huyo kuondoka na kurejea Trump Tower saa
21:41.
Hatua ya kutofuata desturi na kutowafahamisha wanahabari
wanaomfuatilia rais mteule kuhusu safari hiyo imevitia hofu vyombo vya habari
Marekani
Vyombo hivyo tayari vina wasiwasi kuhusu kunyimwa uhuru wa
kufikia na kuzungumza na maafisa wa Bw Trump, na uwezekano wa kuzuiwa kupata
habari zautawala wake kwa urahisi atakapoingia madarakani.
Bi Hicks baadaye aliwaambia wanahabari kwamba hakufahamu mipango
ya Bw Trump na akaahidi kwamba wanahabari "watapata uhuru wa kufikia maafisa
wa serikali na taarifa za serikali kama ilivyokuwa chini ya marais
wengine".
Chama cha Waandishi wa Habari wa Ikulu ya White House
kimeshutumu kisa hicho. Viongozi wa chama hicho wamesema "haikubaliki kwa
rais ajaye wa Marekani kusafiri bila waandishi wa habar wa kufuatilia habari
zake na kuwafahamisha wananchi kuhusu alipo".
Rais wa chama hicho Jeff Mason hata hivyo amesema amepokea
hakikisho kutoka kwa Bi Hicks lakini akasema wakati wa kutekeleza ahadi hiyo ni
sasa na kusisitiza kwamba "waandishi wa habari wa kumfuatilia rais mteule
wapo...kufuatilia shughuli zake anapoandaa serikali mpya".
No comments:
Post a Comment