Mtoto Happiness Josephat (6)
aliyefanyiwa upasuaji wa kupandikiza betri moyoni katika Taasisi ya Tiba ya
Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), amefariki dunia.
Mama mzazi wa Happiness, Elitruda Malley
amesema Happiness alifariki dunia ghafla juzi mchana.
Alisema Jumapili, mtoto
huyo alikuwa mzima na walikwenda kanisani kutoa sadaka ya shukrani kama ishara
ya kumshukuru Mungu kwa mambo aliyowatendea na wakarudi nyumbani salama.
“Jana tumeamka vizuri lakini ghafla
hali yake ilibadilika akaanza kulalamika kuwa anajisikia vibaya, tukamkimbizia
Hospitali ya Selian hapa Arusha lakini tukiwa njiani alifariki dunia,” alisema.
Elitruda alisema kifo cha mwanawe
kimemhuzunisha mno na daima atamkumbuka.
“Alikuwa tayari amesharudi shuleni,
alikuwa akiniambia kuwa atasoma kwa bidii ili ndoto yake ya kuwa daktari bingwa
itimie aweze kusaidia watu wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali,” alisema.
Hata hivyo, alisema maziko ya
Happiness yanatarajiwa kufanyika leo huko Mbulu mkoani Manyara.
Mkurugenzi wa JKCI, ambako
Happiness alifanyiwa upasuaji, Profesa Mohamed Janabi amesema taarifa hiyo
imemshtua ikizingatiwa mtoto huyo alikuwa anaendelea vizuri.
“Sikuwa na taarifa, nitawasiliana
na mama yake tujue hasa shida gani ilitokea, maana zipo sababu
nyingi labda alipita jirani na mitambo ya umeme au simu, hizo ni sehemu
hatarishi kwa mtu aliyewekewa betri kwenye moyo,” alisema.
Happiness alifanyiwa upasuaji huo
wa historia nchini Julai 15, mwaka huu katika Taasisi ya JKCI wa kuwekewa betri
maalumu kwenye moyo ambayo kitaalamu inaitwa ‘pacemaker’.
Kwa mujibu wa madaktari waliokuwa
wakimtibia mtoto huyo, wakati alipopekekwa hospitalini hapo, mapigo yake ya
moyo yalikuwa 20.
Walisema hali hiyo kwa mtoto
si ya kawaida kwa vile anapaswa kuwa na wastani wa mapigo 60 hadi 100 kwa
umri wake.
Mtoto Happiness alizaliwa na tatizo
hilo ambalo mara nyingi hali hiyo huwakumba watu wazima.
Moja ya ndoto za mtoto huyo ambayo
alinukuliwa akiisema ni kuwa daktari bingwa wa kutibu magonjwa mbalimbali.
No comments:
Post a Comment