Mwanamke mkazi wa Unga-Limited jijini hapa, Lightness Kivuyo
ameripotiwa kufa wakati akifanyiwa maombi nyumbani kwa mchungaji aliyejulikana
kama ‘Nabii Rajabu’ eneo la Kwa-Mrombo pia jijini hapa.
Kwa
mujibu wa dada wa marehemu, Juliana Kivuyo, Lightness alikuwa amesindikizwa
nyumbani kwa nabii huyo nyakati za usiku na mumewe aliyemtambulisha kama Shafii
Mohammed na kwamba wakati akifanyiwa ibada ya maombi, alianguka na kufariki
miguuni mwa ‘Mtume,’ huyo.
“Baadaye shemeji alikuja nyumbani
akihema, huku anadai kuwa dada alikuwa kwenye hali mbaya kule kwenye maombi,”
alisema Juliana na kuongeza kuwa alitoka mbio kwenda Kwa-Mrombo nyumbani kwa
Nabii Rajab na kumkuta dada yake amelazwa kwenye kochi, akiwa bila nguo
isipokuwa tu khanga alizofunikwa nazo.
Nabii huyo pia anadaiwa kumnyoa
nywele zote pamoja na nyusi za macho wakati akimfanyia ‘huduma,’ hiyo.
Polisi jijini hapa wamethibitisha
tukio hilo wakiongeza kuwa tayari watu wawili wamekamatwa kutokana na kifo
hicho cha ‘maombi tatanishi.’
Aidha, Kamanda wa Polisi wa Mkoa,
Charles Mkumbo ameongeza kuwa atatoa taarifa kamili mara baada ya kikao chake
na Mkuu wa Mkoa.
Mganga Mkuu katika Hospitali ya
Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Jacqueline Uriwo amekiri kupokea mwili wa
marehemu, lakini akasema, “Kwanza walijaribu kutudanganya kuwa huyo mama
alikuwa hai na kwamba aliletwa kwa ajili ya matibabu, lakini tukagundua kuwa
walichokileta ni mwili mfu, hivyo tukampeleka kwenye chumba cha kuhifadhi
maiti!.”
Mkurugenzi wa Huduma ya Mazishi
katika hospitali hiyo ya mkoa, Dk Francis Coster alisema mwili ulipelekwa hapo
na mume wa marehemu ambaye alisisitiza kuwa mkewe hajafa, bali kazimia tu na
kwamba mara nyingi huzimia kwa saa nyingi.
Dk Coster aliongeza kuwa ilibidi na
wao wasiweke mwili kwenye jokofu na kuulaza kwenye machela kwa saa sita na
ndipo wakaamua kuuweka kwenye droo za maiti, kwani ilikuwa wazi sasa kwamba
asingeamka tena asilani.
Waganga hospitalini hapo wamekiri
kuwa mwili wa marehemu uliletwa hospitalini hapo ukiwa umenyolewa upara, lakini
ukiwa na mikwaruzo pamoja na uvimbe hususan maeneo ya mikono na kifua.
Baba mkubwa wa marehemu, Ally
Kivuyo ambaye ndiye mlezi wa Lightness, alisema mume wa marehemu alimtaarifu
juu ya kifo hicho na kuongeza; “Lakini baadaye nikaletewa taarifa nyingine kuwa
Lightness kumbe alikufa wakati akifanyiwa maombi au vitu vingine, nyumbani kwa
mtu anayeitwa ‘Nabii Rajabu,’ hapo basi ikabidi niwataarifu polisi ambao
walikuja kumkamata mumewe pamoja na huyo anayejiita nabii au mtabiri.
Source: Habari Leo
No comments:
Post a Comment