Serikali imewalaumu wazazi
kuwa ni chanzo cha kushuka kwa maadili miongoni mwa wanafunzi, kwa kuwa kama
walezi, hawana ushirikiano mzuri na walimu.
Kutokana na hali hiyo, imesema
walimu wameacha kurekebisha maadili ya wanafunzi kwani hawaungwi mkono,
hivyo kuwaongezea kiburi wanafunzi.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es
Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa,
Joyce Ndalichako kwenye ufunguzi wa mdahalo kuhusu kujenga na kukuza maadili,
haki za binadamu, uwajibikaji utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa.
Mdahalo huo ni sehemu ya
maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu ambayo yatakafikiwa kilele
Desemba 10 mwaka huu.
Kuhusu maadili aliwaomba wazazi na
walimu kuweka misingi bora ya malezi kwa wanafunzi kuzingatia maadili.
“Wazazi watimize wajibu wao wa
kuwalea watoto ipasavyo na wanafunzi mkubali kupokea na kuzingatia mafundisho
ya maadili, kamwe msikubali kuja kufunzwa na ulimwengu,” alisema Profesa
Ndalichako akiwaasa vijana walioko shuleni kuwa watambue hakuna mafanikio bila
nidhamu na bidii.
Aidha, alisema serikali imebaini
kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya walimu kuwa Bodi za Shule zimekuwa
zikipelekewa wanafunzi wakorofi na kuwatetea bila kuchukua hatua na kuwaacha
wakiendelea na masomo.
“Kitendo hiki huwapa kiburi zaidi
wanafunzi hao na kuamua kuwafanyia vitendo viovu vinavyodhalilisha walimu wao,” alisema na
kuwaagiza wakuu wa shule na Bodi zote kuhakikisha wakati wote wanachukua hatua
stahiki dhidi ya utovu wa nidhamu unaofanywa na wanafunzi wao.
No comments:
Post a Comment