Mpango wa kuweka
mashine mpya za kisasa za kukagua mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam ambazo
zina uwezo wa kusoma na kupeleka taarifa na picha za mizigo kwenye mifumo ya
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Mamlaka ya Mapato (TRA) umekamilika.
Kukamilika
kwake kumetokana na maagizo aliyoyatoa Rais John Magufuli kuwa TPA na TRA
zishirikiane kuendesha mashine za kukagua mizigo zinazotoa taarifa na picha
mubashara, pamoja na kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha serikali haipotezi
mapato na kupitisha mizigo haramu.
Kuwepo kwa mashine hizo
kutazisaidia TPA na TRA kubaini shehena zilizoko kwenye makasha yanayofikishwa
bandarini hapo kupelekwa na kutoka nje ya nchi kama inawiana na nyaraka za
mzigo huo, hivyo kutozwa ushuru sahihi kwa mzigo stahiki, Lengo la kufunga
mashine hizo ni kuongeza mapato kwa serikali.
Meneja wa mradi huo, Zhang Sheng
amesema Jumanne hii kuwa mradi huo umekamilika na sasa wako katika hatua ya
pili ya mafunzo na skana hiyo mpya inaweza kutumika muda wowote mara baada ya
kukamilisha mafunzo.
Kwa mujibu meneja huyo kutoka
China, skana hiyo ina uwezo wa kusoma na kupeleka taarifa na picha za mizigo
mubashara kwenye mifumo ya TPA na TRA kwa wakati mmoja bila kuchelewa.
Kutokana na kukamilika kwa mradi
huo, TRA na TPA zimeanza kuwapa mafunzo watumishi wao namna ya kutumia mashine
hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TPA ,
Deusdedit Conatus Vitalis Kakoko, wakati akifungua mafunzo hayo ya siku tano
alizipongeza serikali zote mbili kwa kukamilisha mradi huo.
“Nazipongeza Serikali za Tanzania
na China kwa kuwezesha mradi huu kukamilika. Tunatarajia mafunzo hayo
yatawaongeza uwezo wafanyakazi, ufanisi wa bandari pamoja na kuongeza mapato ya
Serikali,” alisema Kakoko.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo
baada ya kubaini kuwa kati ya mashine nne za ukaguzi wa mizigo zilizopo, ni
mashine mbili tu ndizo zinafanya kazi na hazina uwezo wa kukagua mizigo yote
inayotoka na kuingia nchini kupitia bandari hiyo hali inayosababisha kutokuwepo
kwa udhibiti wa uhakika wa udanganyifu.
BY: EMMY MWAIPOPO
No comments:
Post a Comment