RAIS John Magufuli amefichua siri
ya hatua yake ya kuitumbua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA).
Amesema alilazimika kuchukua hatua
hiyo baada ya bodi hiyo kuidhinisha Sh bilioni 26 kupelekwa kuwekwa kwenye
akaunti maalumu( Fixed Account) katika benki kadhaa za biashara.
Bodi hiyo ilitoa idhini ya
kupelekwa fedha hizo katika benki hizo wakati kuna agizo la Rais la kupiga
marufuku kwa taasisi za umma, mashirika ya umma, idara za serikali, wakala na
wizara kuweka fedha zao katika benki za kibiashara.
Fedha hizo zinatakiwa zifunguliwe
akaunti katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Jumapili iliyopita asubuhi, Ikulu
ilitangaza kwamba Dk Magufuli ameivunja Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, na saa
chache akateua Naibu Kamishna Mkuu mpya.
Ikulu bila kueleza sababu, ilisema
kwamba Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya
TRA, Bernard Mchomvu na kuivunja bodi nzima.
Aidha, pamoja na kuivunja bodi hiyo
alimteua Charles Kichere kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, kuziba nafasi
iliyokuwa wazi kwa mwaka mmoja baada ya Dk Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa
akishikilia wadhifa huo Lusekelo Mwaseba.
“Uteuzi wa Mwenyekiti mwingine wa
Bodi ya Wakurugenzi wa TRA na Bodi ya Mamlaka hiyo utatangazwa baadaye,” ilieleza taarifa
ya Ikulu iliyotolewa Jumapili asubuhi sana.
Akihutubia jana katika Mahafali ya
31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwenye Makao Makuu ya chuo hicho,
Bungo wilayani Kibaha katika mkoa wa Pwani, Dk Magufuli alisema aliitumbua bodi
hiyo kutokana na kukiuka taratibu.
Alieleza kuwa kitendo chao cha
kuidhinisha fedha hizo kuwekwa kwenye benki tofauti, ni tofauti na maelekezo
kwani huo ndio ulikuwa mchezo unaofanywa na taasisi na mashirika mbalimbali.
“Sasa sifahamu kama Chuo Kikuu
Huria na nyinyi mmekuwa mkiweka fedha za maendeleo katika Fixed Deposit
Account, (akaunti maalumu) lakini huo ndio umekuwa ni mchezo, juzi hapa
tumekuta fedha kiasi cha Shilingi bilioni 26 zilizokuwa zimetolewa na Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya matumizi ya TRA, zikapelekwa kwenye benki
tatu kama Fixed Deposit Account na Bodi ya TRA ikapitisha, ndio maana
nilipozipata hizo taarifa, fedha nikachukua na Bodi kwa heri.
“Hata kwa sasa hivi Waziri
(wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako) upo hapa, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)
ambayo ilianzishwa kwa sababu maalumu, inachangiwa fedha wakati kuna fedha zao
wameziweka kwenye Fixed Deposit Account, Waziri hiyo ni message sent and
Delivered,” alisisitiza Rais Magufuli.
Alisema kumekuwa na mchezo wa wakuu
wa taasisi mbalimbali kuchukua fedha na kuziwekwa kwenye akaunti maalumu ambako
serikali inakwenda kukopa kwa gharama kubwa.
“Kwa sasa huu ndio mchezo ambao
unachezwa na kuisababishia serikali kukosa fedha jambo ambalo serikali haiko
tayari kuona matumizi mabaya ya fedha zake,” alieleza Dk
Magufuli ambaye anafahamika kwa kusisitiza kubana matumizi ya serikali na
kukerwa na ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji wa serikali.
Alisema mchezo huu umekuwa ukiipa
serikali gharama kubwa kwa sababu ya kukopa fedha kwenye benki kwa gharama
kubwa na kupotosha upatikanaji wa mapato.
“Naomba mtuombee tuendelee kutumbua
kwani nchi ilifika mahali pabaya ambapo wanaweza kuitisha vikao hata Ulaya na
kutokana na tumbua hii mapato yameongezeka kutoka trilioni 1.2 na kufikia 1.8
ambapo uchumi umeimarika,” alieleza Dk Magufuli.
Alisema uchumi umeimarika na
unatakiwa ukue kwa asilimia 7.2, lakini hadi robo ya mwaka huu umekua kwa
asilimia 7.9 na kuwa moja ya nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi, ambazo
kati ya nchi tano imekuwa ya pili baada ya Ivory Coast.
Aidha, alisema thamani ya fedha
imepanda na kwamba wanaopotosha juu ya fedha ni wale waliokuwa wanapiga dili
ambao kwa sasa hawana nafasi. Jumla ya wahitimu 4,027 walihitimu na kutunukiwa
shahada mbalimbali na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Waziri Mkuu mstaafu
Mizengo Pinda.
No comments:
Post a Comment