Serikali imesema kuna Watanzania wengi wanaoishi Marekani kinyume cha
sheria, lakini haijui idadi yao wakati Rais mteule wa nchi hiyo, Donald Trump
akisubiriwa kutekeleza ahadi yake ya kutimua wahamiaji haramu.
Kuchaguliwa
kwa Trump kuwa Rais wa 45 wa Taifa hilo kubwa, kumeibua hofu miongoni mwa kwa
mataifa mbalimbali kuhusu raia wao wanaoishi bila ya nyaraka halali kutokana na
sera za mfanyabiashara huyo maarufu za kutotaka wageni haramu.
Awali, Serikali ya Rais Barack
Obama ilitoa ahueni kwa watu wanaosadikiwa kuwa milioni 11.1 (kwa mujibu wa
takwimu za mwaka 2014 za taasisi ya utafiti ya Pew ya Marekani) baada ya
kuwaruhusu kupitia mchakato ambao ungewapa uhalali wa kuishi nchini humo.
Lakini katika kampeni zake, Trump
alisema hahitaji wageni walioingia Marekani kwa kukwepa sheria na hivyo
atawatimua ili wakaanze mchakato wa kuomba kuingia Marekani wakiwa kwenye nchi
zao.
Akizungumza na Mwananchi juzi,
Kaimu Mkuu wa Idara ya Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje, Robi Bwiru alisema:
“Kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaoishi Marekani lakini kwa kuwa suala la mtu
kutaka kutambulika na ubalozi wake ni la hiari, hatuna idadi kamili ya
Watanzania ambao wapo kule bila nyaraka halali.”
Kuhusu misimamo ya kiongozi huyo
kutoka chama cha Republican dhidi ya nchi za Afrika, Bwiru alisema Tanzania
haiwezi kutoa msimamo wowote kabla ya kuona utekelezaji wa ahadi zake.
Kwa mujibu wa taasisi ya utafiti ya
Pew, Wamexico ndiyo wanaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wageni wanaoishi
bila ya nyaraka halali wakiwa asilimia 52, lakini kutokana na uchumi wa Mexico
kuimarika pamoja na ulinzi mkali mpakani, idadi yao inapungua.
Badala yake, watu kutoka Kusini mwa
Jangwa la Sahara, ikiwamo Tanzania, wameongezeka katika kipindi cha miaka sita
iliyopita.
Pew inakisia kuwa idadi ya wageni
kutoka Afrika wanaoingia isivyo halali imeongezeka hadi kufikia asilimia 37.5,
wakati kutoka barani Asia imeongezeka hadi asilimia 11.5 na kutoka Amerika ya
Kati ni asilimia 6.3. Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment