Mwanasiasa mkongwe na waziri wa
zamani wa Serikali ya awamu ya kwanza hadi ya nne, Joseph Mungai, amefariki
dunia.
Mungai aliyezaliwa Oktoba 24,1943
alifariki dunia Dar es Saalam jana baada ya kuugua kwa muda
mfupi.
Akisimulia mazingira ya kifo cha
baba yake, mtoto wa marehemu, William Mungai, jana alisema baba yake alifariki
dunia wakati akipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu.
Alisema kabla ya kifo hicho baba
yake alianza kulalamika kuumwa na tumbo na kutapika ambako alipelekwa katika
hospitali moja ambayo hakutaka kuitaja.
Alisema baada ya kufikishwa
hospitalini hapo, hali yake ilizidi kubadilika na kuwa mbaya zaidi na hivyo
wakaamua kumkimbiza Muhimbili kwa matibabu zaidi.
“Ni kweli baba amefariki dunia saa
10 jioni leo (jana) wakati tukimpeleka Muhimbili baada ya kulalamika kuumwa na
tumbo. Hivi tunavyoongea, ndiyo tunatoka Muhimbili ila taarifa zaidi
tutawapatia baada ya kikao cha ndugu,” alisema William kwa kifupi.
Ingawa William hakutaka kuzungumzia
kifo hicho kwa undani, taarifa zilizopatikana na ambazo hazijathibitishwa,
zinasema kiongozi huyo alikunywa kinywaji katika hoteli moja maarufu ya
Dar es Salaam.
Watu walio karibu na familia ya
Mungai mameeleza kuwa, jana mchana Mungai alikuwa katika hoteli hiyo
iliyopo Msasani akipata kinywaji kwa kuwa alikuwa na mazoea ya kufika mahali
hapo.
“Mzee jana alikuwa katika hoteli hiyo akiendelea
na kinywaji akipendacho cha whisky. Inasemekana baada ya kutoka hotelini hapo
na kurudi nyumbani kwake, alianza kutapika huku akilalamika kusikia maumivu
makali ya tumbo.
“Vijana wake walimpeleka hospitali
ya karibu, lakini hali ilizidi kuwa mbaya ndipo familia iliamua kumkimbiza
Muhimbili ambako aliaga dunia,” alisema mtoa taarifa huyo
ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Mungai aliwahi kuwa Mbunge wa
Mufindi kupitia CCM kwa miaka 35.
Pia amewahi kushika nyadhifa
mbalimbali serikalini enzi za utawala wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere na pia katika awamu za pili, tatu na nne.
Baadhi ya nyadhifa alizowahi
kushika kwa nyakati tofauti ni uwaziri wa iliyokuwa Wizara ya Elimu na
Utamaduni, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo na Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi.
No comments:
Post a Comment