Baadhi ya Viongozi na wanachama wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar wametakiwa kuacha tabia ya kutumia mitandao
ya kijamii kujadili masuala yanayohusu Chama badala yake watumie vikao halali
vinavyotambuliwa na Katiba ya Chama hicho.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu
Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai wakati akifunga Mkutano wa Viongozi wa
Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kusini Unguja Kichama uliofanyika katika Shule
ya Msingi Makunduchi Mkoani humo.
Alifafanua kwamba tabia hiyo
ya kujadili, kukosoa na kuwatuhumu baadhi ya viongozi wa ngazi mbali mbali wa
Chama na Jumuiya zake kupitia Mitandao ya kijamii ni utaratibu unaokwenda
kinyume na miongozo ya chama hicho.
Alisema Katiba ya CCM
inaelekeza Kwamba mambo yote yanayogusa maslahi mapana ya Chama yajadiliwe
Katika Vikao halali vinavyotambuliwa na kanuni za Chama, kwani jukwaa hilo
ndiyo sehemu rasmi ya kukosoana na kupeana maelekezo.
Vuai alisikitishwa na tabia hiyo na
kueleza kuwa njia pekee ya kumaliza Changamoto hiyo ni Wanachama na
Viongozi kujenga utamaduni wa Kusoma na kuelewa Kanuni, Katiba na miongozo
mbali mbali ya CCM ili kufahamu wajibu, majukumu, haki na maadili yanayoongoza
Chama.
Alisema tabia hiyo imekuwa
ikifanyika katika Magroup ya Mitandao ya kijamii zikiwemo Facebook, WhatsApp na
mitandao mingine, jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa kanuni za Chama.
“ Wanachama, Viongozi na Watendaji
naomba muelewe kwamba hiki Chama kinaendeshwa kwa utaratibu maalum
ulioelezwa Kikatiba , Kikanuni na miongozo mbali mbali, kwa nia ya
kulinda hadhi na heshima ya Chama chetu, na hakuna jambo lolote
linaloshindikana kupatiwa ufumbuzi kupitia utaratibu huo.
"Sasa panapojitokeza baadhi ya
Watu miongozi mwetu wakaanza kujadili na kuwakosoa wenzao nje ya mfumo huo basi
hao tunawahesabu kuwa wana nia ya kuanzisha Majungu, Fitna na mpasuko
katika taasisi yetu.”, alieleza Vuai na Kuongeza kuwa CCM ni Chama
imara na kinachoheshimu Demokrasia katika kujadili mambo yake na kuyatolea
maamuzi stahiki katika Vikao rasmi na sio vichochoroni au vibarazani.
Aliongeza kuwa sio kwamba kuna
viongozi na wanachama wanaogopa ama hawataki kukosolewa lakini lazima
heshima na nidhamu iwepo katika kutekeleza matakwa ya Demokrasia ndani ya Chama
hicho kwa kuheshimu utaratibu uliowekwa Kikatiba.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani
ya Uchaguzi ya Chama hicho ya mwaka 2015/ 2020 katika Mkoa huo
aliwapongeza Viongozi wa Majimbo wakiwemo wabunge, wawakilishi na Madiwani huku
akiwasisitiza Viongozi wa Chama kuhakikisha wanakagua kikamilifu miradi inayotekelezwa
na viongozi hao ili kujiridhisha kama inawanufaisha wananchi wote.
Aliwataka viongozi wa Chama na
Jumuiya zake kuwa wa kwanza kutambua kero na changamoto za wananchi wa maeneo
mbali mbali na waziwasilishe kwa Wakuu wa Wilaya (DC) ili ziweze kupatiwa
ufumbuzi wa kudumu na Serikali.
“ Huu sio wakati wa kusubiri
taarifa zinazohusu Changamoto za Chama, Jumuiya na Serikali ziletwe Ofisini,
badala yake mtoke na kuzitafuta wenyewe ili kuwasaidia wanachama na wananchi
kutatuliwa kero zao kwa haraka kupitia Mamlaka husika.”, alisisitiza Vuai.
Alisema Viongozi wanatakiwa
kufahamu kwamba suala la kuwatumikia wananchi sio jambo la hiari bali ni lazima
watekeleze kwa vitendo ahadi walizotoa wakati wa kampeni kwani wasipotekeleza
Wajibu wao vizuri kwa jamii mwisho wa siku kitakacho hukumiwa ni Chama na sio
kiongozi husika.
Aidha aliwakumbusha viongozi hao
kwamba Chama na Jumuiya zake wanatarajia kufanya Uchaguzi mwaka 2017, hivyo
waanze mapema kuwaelimisha, kuhamasisha na kuwaandaa kisaikolojia wanachama wa
Chama hicho juu ya matumizi sahihi ya kanuni za UChaguzi ili kuepuka lawama
zisizokuwa za lazima.
Alisema Wanachama wanatakiwa
kuwachagua viongozi wenye sifa na wasiokuwa na Mukhari( kuoneana haya) katika
kusimamia mambo ya msingi ya CCM na waumini wa kweli wa Mapinduzi ya
Zanzibar ya mwaka 1964, Muungano wa Serikali mbili wenye vigezo hivyo ndio
wanaofaa kuwa viongozi.
Hata hivyo aliwapongeza Rais wa
Zanzibar, Dkt. Shein na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Magufuli kwa juhudi na kasi zao za kufanikisha mipango ya maendeleo ya
nchi kwa ufanisi mkubwa hali inayoongeza hamasa kwa jamii kuendelea kuwaamini.
No comments:
Post a Comment