Wabunge wamegomea hatua ya
Serikali kutaka kusimamia posho na marupurupu yao, huku wakitaka suala hilo
waendelee kujipangia wenyewe.
Msimamo huo uliotolewa na Kamati ya
Bunge ya Katiba na Sheria, umetolewa baada ya Serikali kuwasilishwa
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba tatu ya mwaka 2016.
Awali Serikali ilitaka suala la
stahiki hizo kwa watumishi wa umma liamuliwe na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais
Utumishi na Utawala Bora.
Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya
Katiba na Sheria, Mohammed Mchengerwa, alisema wametoa pendekezo hilo
katika Sheria ya Utumishi wa Umma sura 298 kulinda
dhana ya mgawanyo wa madaraka.
“Tume ya Utumishi wa Bunge na Tume
ya Utumishi wa Mahakama zipewe uhuru kusimamia upangaji wa mishahara,
posho na marupurupu mengine,” alisema.
Akizungumzia mikopo kwa wanafunzi
wa elimu ya juu, alisema kifungu cha 18 cha Muswada huo kuhusu muda wa
mnufaika kurejesha mkopo, Mchengerwa alisema kamati inashauri mkopo
uwe mwaka mmoja baada ya kumaliza masomo.
Alisema hali hiyo itasaidia kutoa
fursa kwa mnufaika kuanza kulipa mkopo wake, utaratibu ambao
hutumika katika nchi nyingine kama Kenya na Zambia.
“Kuhusu wanufaika waliojiajiri
kamati inapendekeza kiwango cha kurejesha mkopo kisipungue Sh 100,000 badala ya
Sh 120,000 kama Serikali ilivyopendekeza,” alisema Mchengerwa.
Awali, akiwasilisha hotuba ya
mabadiliko ya sheria hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju,
alisema kifungu cha 8 cha Sheria hiyo kinaanisha mamlaka ya Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais (Utumishi) kuwa ni pamoja na kufanya uchunguzi kwa ajili ya
kuendeleza ufanisi wa utumishi wa umma.
Alisema Ibara 24 ya Muswada huo
inapendekeza kuongeza kifungu kipya cha 9A cha Sheria kinachoweka masharti kuwa
Taasisi, Wakala au Tume za Serikali hazitakuwa na mamlaka ya kuidhinisha
mishahara na marupurupu kwa watumishi wa taasisi hizo na badala yake kibali kwa
ajili hiyo kitatolewa na Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais (Utumishi).
“Marekebisho hayo yanalenga kuwa na
mamlaka moja inayoratibu mishahara, posho na marupurupu na watumishi katika
taasisi za Serikali na pia kuwianisha mishahara posho na marupurupu mengine kwa
watumishi wa taasisi hizo.
“Masharti yaliyopendekezwa
hayatatumika. Ibara hiyo imefutwa na kuandikwa upya masharti yanayopendekezwa
hayatatumika kwa mishahara, marupurupu na masilahi mengine kwa Bunge,Mahakama,
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),Polisi,Magereza,JKT, Jeshi la Zimamoto na
Uokoaji na Idara ya Usalama wa Taifa ili utaratibu huo kuendelea kama ilivyo
sasa katika sheria zinazosimamia taasisi hizo.
“Kifungu cha 20 (1) (c) cha Sheria
ya Utumishi wa umma kinaipa Tume ya Utumishi wa Umma mamlaka ya kutunga kanuni
kuhusu usaili wa watumishi wa umma unaofanywa na tume hiyo,” alisema
Masaju
Awali kifungu cha 8 kilikuwa
kinapendekeza kufanyiwa marekebisho kumpa mamlaka Katibu Mkuu
(Utumishi) kurekebisha na kuwianisha mishahara, posho na marupurupu
mengine kwa watumishi wa umma wakiwamo wabunge na idara ya
mahakama.
Huku ikipendekeza kuongeza kifungu
kipya cha 9A kinachozizuia taasisi za umma, wakala, bodi na tume zisirekebishe
au kuwianisha mishahara, posho na marupurupu mengine kwa watumishi.
Sehemu ya tano inapendekeza
marekebisho katika Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 kwa lengo la kutoa
tafsiri ya neno “recruitment secretariat”, maneno hayo yametumika katika Sheria
lakini hayakuwa yamepewa tafsiri.
Kiama kwa waajiri
Alisema Ibara ya 19 ya Muswada huo,
inapendekeza kufuta kifungu cha 20 na 21,ambacho kilikuwa kinaeleza kwa kuwa si
rahisi mwajiri kufahamu kama mtumishi anayeajiriwa ni mnufaika wa mkopo.
Kutokana na hali hiyo,alisema
Muswada unaainisha kuwa mwajiri atatakiwa kuifahamisha Bodi ya Mikopo ndani ya
siku 28,baada ya mwajiriwa huyo mwenye Shahada au Astashahada ili bodi
iangalie kama mwajiriwa huyo ni mnufaika wa mikopo.
“Mwajiri ambaye atashindwa
kutekeleza masharti ya kifungu hicho atakuwa anatenda kosa la jinai ambalo
adhabu yake ni Sh milioni moja au kifungo cha miezi sita gerezani. Pia
inapendekezwa baada ya mnufaika wa mkopo mwajiri atatakiwa kukata asilimia 15
ya mshahara wa mwajiriwa.
“Bodi au mawakala wake wawe na
mamlaka ya kukagua kumbukumbuku za waajiriwa kwa lengo la kufuta taarifa
zinazohusiana na wanufaika wa mkopo pamoja na kumbukumbu za waajiriwa kwa
lengo la kutafuta taarifa zinazohusiana na wanufaika wa mkopo kwa hatua zao
muhimu kuhusu makusanyo wa mikopo,” alisema
AG Masaju alisema kifungu cha 57
cha sheria hiyo, kinaweka masharti kuhusu zuio kwa shughuli za binadamu
zinzoathiri ulinzi wa bahari, mito, mabwawa zisifanyike ndani ya mita 60 kutoka
kingo za bahari, mito au mabwawa.
Alisema hatua hiyo imekusudiwa
kuimarisha ulinzi na usalama wa mazingira ya maeneo husika ya bahari, maziwa na
mito na mabwawa.
“Ibara ya 11 ya Muswada
inapendekeza kifungu hicho kirekebishwe katika kifungu kidogo cha pili
kuweka mwongozo wa namna ya kupima mita 60 ambako shughuli za binadamu
zimezuiliwa kufanyika.
“Kifungu cha 184 kinaeleza athari
na uthamini wa mazingira. Ibara ya 12 inapendekeza kuwa kitendo cha mtu yeyote
kushindwa au kukataa kufanya tathimini ya athari za Mazingira kwa mradi
unaohitaji tathmini hiyo kufanyika ni kosa la jinai ambalo adhabu yake ni faini
isiyopungua Sh milioni tano na isiyozidi Sh bilioni moja au kifungo
kisichopungua miaka miwili,” alisema.
No comments:
Post a Comment