Wafuasi wa Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif
Hamad jana waligeuka sinema ya bure baada ya kutwangana makonde hadharani
katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Ugomvi huo ulioibua mapambano ya
ngumi ulitokea jana baada ya wafuasi wa Maalim Seif waliokuwa mahakamani hapo
kumzuia Profesa Lipumba kuingia kusikiliza kesi inayomkabili iliyofunguliwa na
Baraza la Wadhamini wa Chama hicho.
Profesa Lipumba alifika mahakamani
hapo saa mbili asubuhi, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kesi hiyo dhidi yake
kufunguliwa ikidai kuwa yeye si mwanachama halali wa CUF.
Baada ya kesi za Jaji Sakiet Kihio
kuitwa na mtoa matangazo wa Mahakama kwa kuelekeza kuwa kesi za Jaji huyo
zinasikilizwa chemba watu wote waliinuka na kuelekea katika chumba hicho
wakiwamo mawakili wa pande zote.
Walipofika kwenye mlango wa chumba
cha Mahakama, wafuasi wa Maalim Seif walisimama mlangoni kumzuia Profesa
Lipumba kwa madai kuwa wanaotakiwa ni mawakili tu na si watu wengine, ndipo
wafuasi wa Mwenyekiti huyo walipoingilia kati na kuwashushia kipigo watu hao.
Hatua hiyo ilishuhudia mabadilishno
ya makonde na kusababisha watu wawili upande wa Maalim Seif kuumia,
na kusababisha Jaji Kihio kutoa amri kuwa waingie mawakili na walalamikiwa
ndipo Lipumba naye akaingia.
Kesi iliendelea kusikilizwa, huku
askari wakiimarisha ulinzi wa chumba hicho, kwa sababu wakati wafuasi hao
wanapigana wao hawakuwapo. Jaji Kihio aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 6
zitakaposikilizwa sababu za Bodi hiyo kumtaka ajitoe kusikiliza kesi hiyo.
Baada ya kesi hiyo kuahirishwa,
Profesa Lipumba alitolewa na wafuasi wake akiwa chini ya ulinzi mkali kwa
kuhakikisha kuwa hakuna mtu atakayemgusa na alipofika nje, alipokewa na wafuasi
wengine wakiwa na mabango yenye ujumbe dhidi ya Maalim Seif.
Bango moja liliandikwa: ‘Maalim
Seif kama ulikaa na CCM umeshindwaje kukaa na Mwenyekiti wako Lipumba
mkayamaliza’, lingine: ‘Maalim Seif tulijua CCM ndiyo kiboko yako, kumbe
Lipumba ndiye mwamba wako’, huku wakiendelea kuimba wimbo wa chama hicho.
Lipumba alipoingia kwenye gari
alishusha kioo na kusalimu wafuasi wake kwa kuwapungia mikono, huku wengine
wakisukuma gari lake kabla ya kuondoka eneo la Mahakama.
Hata hivyo, Profesa Lipumba
hakutaka kuzungumza chochote, akitumia muda wake mwingi kutabasamu na kupunga
mkono. Wakati hayo yote yakifanyika, nje ya Mahakama askari walikuwa tayari
wametenga makundi hayo mawili, lakini bila kufanya hivyo, watu hao wangeendelea
kupigana.
Wakili wa Bodi hiyo, Juma Nassoro
akiwa nje ya Mahakama, alimkariri Jaji akisema Desemba 6 kesi hiyo
ataisikilizia kwenye Mahakama ya Wazi, kwa sababu alikuwa hajui kama watu ni
wengi, kwa hiyo hataifanyia tena chemba.
Pia alisema Profesa Lipumba,
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
George Masaju na wafuasi 11 wamewasilisha pingamizi mahakamani hapo, kuwa
wateja wake walifungua kesi hiyo bila idhini ya Mahakama na pia Maalim Seif
alibariki kufunguliwa kwa kesi hiyo bila idhini ya Bodi.
Baadaye mawakili wa CUF, Nassor na
Hashimu Mziray waliwasilisha ombi la kumtaka Jaji Kihiyo ajitoe kusikiliza
shauri hilo kwenye Mahakama hiyo, na sababu za kumkataa zitaelezwa Desemba 6
saa saba mchana wakati kesi hiyo itakapokuja kusikilizwa.
Walalamikaji hao wanaomba Mahakama
itengue barua ya Msajili ya kumtambua Profesa Lipumba kuwa mwanachama hai wa
CUF. Wakili Mziray alisema walifungua kesi hiyo kwa hati ya dharura
kutokana na mambo yalivyo sasa ndani ya chama hicho, kwa sababu hawajui hata
ofisi zingine zinaendeshwaje.
Alisema katika maombi hayo,
wanaiomba Mahakama mambo matatu, ambayo ndiyo yanasababisha kufukuta kwa
mgogoro, kwa hiyo wanaomba yatenguliwe ili shughuli za kisiasa ziendelee.
Alisema mambo hayo ni pamoja na
Mahakama kutengua barua ya Msajili ya Septemba 23 ambayo ilitengua uamuzi wa
CUF wa kumfukuza uanachama Profesa Lipumba na kumhalalisha kuwa mwanachama hai
wa chama kama Mwenyekiti.
No comments:
Post a Comment