Wakili wa Serikali, Patrick Mwita
amemuomba radhi Hakimu Mkazi Mkuu wa Kisutu kwa kushindwa kutekeleza amri ya
kumkamata mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anayekabiliwa na
kesi ya uchochezi pamoja na wahariri wa gazeti la Mawio.
Wakili Mwita alifanya hivyo jana
baada ya hakimu huyo, Thomas Simba kumuhoji sababu za kushindwa kutekeleza amri
hiyo wakati hati ya kumkamata ilitolewa Novemba 3, 2016 na wakili huyo
kuisaini. “Kwa nini hamkumkamata” Si mlikuwa na wajibu wa kumkamata? Mnamuogopa?”alihoji
hakimu huyo.
Hata hivyo, pamoja na kuomba radhi
hiyo mahakama imechukua hati ya kusafiria ya Lissu ili kudhibiti safari zake
nje ya nchi kwa kuwa amekuwa akisafiri bila kuitaarifu mahakama.
Katika kesi hiyo, Lissu na watu
wengine watatu wameshtakiwa kwa makosa matano ya uchocheza kutokana na habari
iliyochapishwa na gazeti la Mawio kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar.
Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo
hadi Novemba 28, 2016 na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.
Kabla ya uamuzi huo, Wakili Mwita
alisema jana ilikuwa siku ya kesi hiyo kutajwa na kwamba upelelezi unakaribia
kukamilika.
Kuhusu madai ya kudharau mahakama
Wakili Peter Kibatala anayemwakilisha Lissu aliiambia mahakama kuwa mteja wake
yupo mahakamani, hivyo ametii amri ya mahakama na kwamba jukumu la dhamana ni
kuhakikisha mshtakiwa anakuwapo mahakamani wakati wa kesi yake na kwamba uwepo
wake ni kutii masharti ya dhamana.
Hata hivyo, Wakili Mwita alidai
kuwa kitendo cha Lissu kutofika mahakamani mara mbili mfululizo ni kama
kuonyesha dharau kwa mahakama hiyo.
Mwita alidai kuwa Lissu ni
mwanataaluma wa sheria na anafahamu taratibu za kufuatwa kama hafiki mahakamani
na kwamba mdhamini si mbadala wa mshtakiwa mahakamani.
“Alipaswa kuandika barua kuitaarifu
mahakama hii kama wakili kuwa ana kesi ya uchaguzi anayoiendesha Bunda na
kuambatanisha na samansi ama orodha ya kesi. Tunaomba mahakama iheshimiwe na
jukumu la kumfutia dhamana ama kutokumfutia dhamana Lissu bado lipo mikononi
mwako mheshimiwa,” alieleza wakili huyo wa Serikali.
Akizungumzia hoja hizo, Hakimu
Simba alisema Lissu ni wakili maarufu, msomi na anajua taratibu zote za
mahakama, lakini wadhamini wake wanababaika, hivyo alimtaka aeleze sababu za
kwenda Ujerumani bila kutoa taarifa mahakamani.
Lissu alijibu kuwa hakuwa na nia ya
kuidharau mahakama, wala kuikimbia kesi inayomkabili bali alikwenda Ujerumani
katika mazingira ya dharura.
Hakimu Simba alimwambia mahakama
inafahamu kesi za uchaguzi na maelekezo yake, hivyo ikamuuliza sababu za
kutotoa taarifa wakati alipokwenda kushughulikia kesi ya Bunda
“Nilipopata taarifa ya kwenda
kuiendesha kesi hiyo ilikuwa ni siku moja baada ya kutoka nchini Ujerumani na
kwamba niliandika barua ya kuitaarifu mahakama na nilituma iletwe mahakamani
kupitia wasaidizi wangu,”alisema Lissu.
Lakini Hakimu Simba alisema: “Hakuna
barua iliyotufikia. Usituingize katika migogoro kutokana na nafasi yako katika
jamii ya mwanasheria. Hatukuogopi labda upande wa mashtaka ndio wamekuogopa.
“Tunataka kufuata mfumo,
hatutakuogopa na wala hatutakuonea. Hapa naona upande wa mashtaka wanapiga blaa
blaa, tuelewane tunaichukua hati yako ya kusafiria ili ukitaka kusafiri tujue.”
No comments:
Post a Comment