Wakati polisi wakisema kuwa
wanaufanyia mchakato wa vipimo vya vinasaba (DNA), mwili wa mtu anayedaiwa
kuuawa nje kidogo ya mji wa Moshi na kuwekwa kwenye kiroba na kuchomwa moto,
familia ya Ben Saanane, msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye
hajulikani aliko imesema inaenda kuuangalia mwili huo.
Hatua hiyo ya polisi kupima DNA
ilielezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa baada ya
hadi jana, mwili huo kutotambuliwa.
Mauaji hayo yaligunduliwa Ijumaa
iliyopita, baada ya watu waliokuwa na gari ndogo ambao hawajafahamika, kumchoma
moto mtu huyo katika Kijiji cha Ongoma na kisha kutoweka kusikojulikana.
Kamanda Mutafungwa aliwaambia
waandishi wa habari jana kuwa mtu huyo hajafahamika na wala hakuna mtu
aliyejitokeza kuutambua mwili huo hivyo kulilazimu jeshi kufanya uchunguzi huo
wa kisayansi.
Kamanda Mutafungwa alitoa wito kwa
ndugu, jamaa na marafiki waliopotelewa na ndugu, wafike katika Hospitali ya
Rufaa ya KCMC kuutambua mwili huo.
Kuhusu madai ya marehemu kwamba
alikuwa amevaa suruali inayofanana na sare za wafungwa, Kamanda Mutafungwa
alisema si kweli kwani nguo iliyoonekana ni blanketi jepesi la rangi ya
chungwa.
Mzazi wa Saanane
Wakati polisi ikijiandaa kwa mchakato
huo, baba wa Saanane, Focus Saanane, jana alikuwa anajiandaa kwenda KCMC
kuangalia mwili huo.
Akizungumza jana mjini Moshi,
Saanane alisema japokuwa mtoto wake alipotelea Dar es Salaam, watakwenda
kuuangalia mwili huo ili kujiridhisha.
Juzi Saanane alikaririwa akiiomba
Serikali kufanya uchunguzi wa kupotea kwa mwanaye akisema ndiyo pekee yenye
vyombo vya kiuchunguzi.
Kuokotwa kwa mwili huo
kunashabihiana na tukio la kupatikana kwa miili mingine saba katika Mto Ruvu
mkoani Pwani ikiwa imefungwa katika viroba na kuwekewa mawe ili izame.
Miili hiyo ilizikwa na wananchi
wanaoishi jirani na mto huo bila kufanyika kwa vipimo vya DNA wala kutoa
tangazo la watu waliopotolewa na ndugu zao kujitokeza kutambua maiti hizo hali
iliyoibua utata.
Tayari Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
alishaagiza kufanyika kwa uchunguzi wa miili hiyo na kutaka wale wote
waliohusika na mauaji hayo watafutwe na kukamatwa.
No comments:
Post a Comment