WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk
Harrison Mwakyembe amesema serikali inatarajia kujadili kushusha kiwango cha
fedha kinachohusika katika makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kwenye mahakama
ya mafisadi ili kukomesha vitendo vya rushwa.
Mwakyembe alitoa kauli hiyo jana
mara baada ya kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda.
“Nimeulizwa sana na waandishi wa
habari tangu Julai hadi sasa walitegemea kungekuwa na kesi nyingi lakini kuna
kesi moja katika Mahakama ya Mafisadi tumekuja kubaini kwamba uchache wa kesi
ndiyo mafanikio makubwa ya hatua ya kisheria tuliyochukua,”amesema.
Aliongeza kwa sasa waliozoea kupora
mabilioni wamerudi nyuma ambapo wezi hao wameonekana wakiiba fedha chini ya Sh
bilioni moja iliyopo kisheria hivyo wanategemea kujadili sheria hiyo ili
iwalenge hata wanaochukua kiasi kidogo.
“Sisi kama serikali tukiona wizi
sasa umenza kupungua na kuenea katika viwango vya Sh milioni 400, 500, 700
tumeanza kujadiliana kuangalia uwezekano wa kushusha kiwango cha fedha ili
tuweze kukomesha kabisa udokozi, ubadhilifu, wizi wa fedha au mali ya umma,”alisema.
Aidha alifafanua uamuzi wa Mkuu wa
Mkoa huo, Paul Makonda kutafuta vijana wanaojua sheria ili kusaidia wananchi
kabla ya kwenda mahakamani ni mzuri.
Aliongeza kuwa tayari wamepeleka
mswada wa msaada wa kisheria ambao utasaidia wananchi hasa wa vijijini na
wanawake ambao ndiyo wanaumizwa na desturi zilizopitwa na muda ili kuwasaidia
kupata haki na itakuwa na wasaidizi wa kisheria nchi nzima wapatao 4,900.
Makonda alisema wamejadili utoaji
na upatikanaji wa haki kwa wakati kwani kuna changamoto ya watu kuwa wengi na
kuchelewa kupata haki zao.
Alisema kwa kuona adha hiyo mkoa
huo kwa kushirikiana na Wakuu wa wilaya watajenga Mahakama za Mwanzo 20 ili
kuongeza kasi za utoaji na upatikanaji wa haki kwa wananchi endapo
wanapopelekwa vituo vya polisi.
No comments:
Post a Comment