WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo kufanya uchunguzi na
kumpelekea taarifa ya watendaji waliohusika katika ubadhirifu wa fedha za ujenzi
wa mradi wa hospitali ya wilaya ya Monduli uliogharimu sh. bilioni 2.7.
Ametoa agizo hilo jana (Jumapili,
Desemba 4, 2016) wakati akizindua hospitali ya wilaya ya Monduli ambayo katika
ujenzi wake kulitakiwa kuwe na jengo la maabara ambalo halipo na fedha
zimeisha.
"Mkuu wa Mkoa shirikiana na
Sekretarieti yako kufanya uchunguzi na atakayebainika kuhusika kwenye
ubadhirifu huu achukuliwe hatua za kisheria kwa sababu ujenzi huu ulihusisha na
jengo la maabara lakini tayari mradi umekamilika na hakuna jengo la
maabara," alisema.
Naye Mkuu wa mkoa huo Bw. Gambo
alisema tayari wameanza kufanya uchunguzi wa ujenzi wa mradi huo baada ya
kubaini kuwa umetumia kiasi cha fedha kilichotumika hakilingani na thamani ya
mradi huo.
Mkuu huyo wa Mkoa aliahidi kufuatilia
suala hilo na uchunguzi utakapokamilika taarifa hiyo itapelekwa kwa Waziri
Mkuu.
Awali, Mganga Mkuu wa Hospitali
hiyo, Zaveri Benela akisoma taarifa ya hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto
ya jengo la upasuaji karibu na wodi ya wazazi hali inayowalazimu kuwasafirisha
wagonjwa umbali wa zaidi ya mita 300 hadi kwenye jengo la upasuaji lililopo
katika majengo ya zamani.
Pia kukosekana kwa jengo la
wagonjwa wa nje na jengo la maabara kwenye majengo hayo mapya hali inayochangia
huduma kutolewa kwenye maeneo miwili tofauti kwa wakati mmoja yaani katika wodi
mpya na majengo ya zamani na hali hivyo inaleta usumbufu kwa wagonjwa.
Katika hatua nyingine Waziri
Mkuu ametoa siku saba kwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Bw. Idd Kimanta
kumaliza tatizo la mgogoro wa ardhi katika kijiji cha Emairete kilichopo
Monduli juu mkoni hapa baada ya kudumu kwa miaka 20.
Mgogoro huo ni wa shamba kubwa
ambalo awali lilikuwa linamilikiwa na kampuni ya bia ya Breweries na
kisha kurejeshwa kwa kijiji hicho ambapo viongozi wa zamani wa
Kijiji hicho walijimilikisha kinyemela.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada
ya kusimamishwa na wanakijiji hao waliokuwa wamebeba mabango ya
kumuomba msaada wa kutatuliwa kwa mgogoro huo wakati anatoka kudhuru
kaburi la Waziri Mkuu wa zamani Hayati Moringe Sokoine.
Waziri Mkuu alimtaka mkuu huyo wa
wilaya kueleza sababu za kwa ya nini uongozi wa wilaya umeshindwa kutekeleza
maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
William Lukuvi ambaye alifika kijijini hapo na kutoa maelekezo.
Baada ya maelekezo hayo Waziri Mkuu
aliwataka wananchi hao kuendelea kuwa na imani ya Serikali ya awamu ya
tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli ambayo ipo kwa
ajili ya kuwasaidia wananchi hasa wanyonge.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo
alikiri kuwepo kwa mgogoro huo kwa miaka 20 na kwamba Waziri Lukuvi alitoa maelekezo
ambayo halmshauri inayafanyia kazi na imeshindwa kuleta majibu kwa wananchi hao
kutokana na ziara ya Waziri Mkuu ambaye aliwataka watekeleze majukumu yao na
wasitumie ziara yake kama kisingizio.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
alisema Serikali na Watanzania wote wanatambua na kuiheshimu kazi nzuri
iliyofanywa na hayati Sokoine kwa Taifa kipindi cha uhai wake na itaendelea
kuienzi. Pia Serikali itaendelea kushirikiana na familia katika mambo
mbalimbali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU
No comments:
Post a Comment