Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed
Shein ameiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuongeza kasi ya kubadili
mitaala katika shule za sekondari na kuingiza somo la ujasiriamali kwa lengo la
kuwaandaa wanafunzi kwa maisha ya kujiajiri.
Pia, alisema Serikali itaimarisha
vyuo vya amali ili somo la ujasiriamali liweze kuchukua nafasi katika mitaala
na kuhakikisha wanafunzi wanapomaliza masomo watoke wakiwa na uelewa mzuri wa
namna ya kujiajiri.
Akizungumza katika kongamano la
siku mbili na maonyesho ya wajasiriamali linalofanyika katika ukumbi wa Baraza
la Wawakilishi, Kikwajuni mjini Unguja, alisema utaratibu huo utawapa elimu
itakayowasaidia kujiajiri watakapokuwa wamemaliza masomo.
Dk Shein aliwakumbusha vijana kuwa
elimu waliyoipata katika vyuo vikuu na taasisi mbalimbali zinazotoa mafunzo ya
kazi na ufundi, wachukulie ni mtaji muhimu katika kuendeleza shughuli za
ujasiriamali.
Hivyo, aliwataka wasijenge dhana
kuwa ujasiriamali ni kufanya biashara ndogondogo za bidhaa zinazoonekana katika
masoko, lakini wajifunze kutokana na uzoefu wa nchi mbalimbali hasa India
ambapo vijana wengi waliosoma wamekuwa wakijiajiri baada ya kumaliza masomo
yao.
Alisisitiza kuwa Serikali inatambua
umuhimu wa kuwaendeleza wajasiriamali katika kuyafikia malengo ya kupambana na
umaskini wa kipato na kupunguza tatizo la ajira, hasa miongoni mwa wanawake na
vijana.
Dk Shein alitumia fursa hiyo
kueleza mafanikio ya Mfuko wa Uwezeshaji ambao katika kipindi cha miaka miwili
tangu ulipoanza umetoa jumla ya mikopo 998 yenye jumla ya Sh1.6 bilioni, kwa
visiwa vyote vya Unguja na Pemba na hadi sasa marejesho ni asilimia 96.
Alisema taarifa zinaonesha kwamba
asilimia 67 ya watu waliopewa mikopo ni vijana wenywe umri kati ya miaka 18
hadi 35, huku akiwataka wanasiasa kutowadanganya vijana kuhusiana suala la
ajira kwani vijana hivi sasa hawadanganyiki.
Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee,
Vijana, Wanawake na Watoto, Maudline Castico alisema kuwa kongamano hilo ni la
kwanza la aina yake kufanyika visiwani humo na kueleza kuwa mchango wa sekta
binafsi kupitia wajasiriamali wakubwa na wadogo ni muhimu ili kufikia lengo la
Zanzibar kuwa na uchumi wa kati ifikapo 2020.
Alisema kuwa kongamano hilo
linatarajiwa kuhamasisha na kuwaelimisha wajasiriamali ili kuendeleza shughuli
zao kwa ufanisi zaidi.
No comments:
Post a Comment