Fundi wa kuziba pancha, Harson
Solomon (38), mkazi wa wilayani hapa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela
baada ya kutiwa hatiani kwa kupatikana na misokoto 601 ya bangi.
Kifungo hicho kimeangukia sheria
mpya ya udhibiti wa dawa za kulevya iliyosainiwa Mei 11, 2015 na aliyekuwa Rais
wakati huo, Jakaya Kikwete. Imeelezwa Solomon ni miongoni mwa washtakiwa wa
mwanzo kufungwa kwa sheria hiyo.
Awali, sheria ilikuwa inatoa mwanya
wa faini na mtu anaposhindwa kulipa ndipo hutumikia kifungo jela lakini hivi
sasa anayepatikana na hatia ya kukutwa na kiwango kikubwa hutupwa jela.
Kifungu cha 11(1) D cha sheria hiyo
mpya, kinaeleza wazi mtu anayezalisha, kumiliki, kuuza, kununua au kusafirisha
dawa za kulevya ikiwamo bangi, adhabu ya chini ni kifungo cha miaka 30
jela.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Joachim Tiganga baada ya kuridhishwa bila kuacha shaka
na ushahidi wa upande wa mashtaka.
Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka
alidai kortini kuwa Desemba 1, 2015 katika maeneo ya Mwika Kimangara, Moshi
Vijijini mshitakiwa alipatikana na kiasi hicho cha bangi.
Pia, anadaiwa kuruhusu eneo
lake kutumika kuuza bangi na gongo.
Akisoma hukumu, Hakimu Tiganga
alisema matumizi ya dawa za kulevya yanazidi kuongezeka nchini na kuathiri
jamii, hivyo Mahakama inatoa adhabu hiyo iwe fundisho kwa wengine.
Katika kipindi chote tangu
afikishwe kortini kwa mara ya kwanza Desemba 11 mwaka jana, mshtakiwa alikana
mashtaka hadi alipotiwa hatiani na kuhukumiwa jana.
No comments:
Post a Comment