Siku moja baada ya mfanyabiashara
Yusuf Manji kuhama kwenye jengo la Quality Plaza, uongozi wa kampuni ya udalali
ya Yono umesema kinachosubiriwa ni mfanyabiashara huyo kulipa deni au kukamatwa
kwa mali zake.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa
Bodi ya kampuni hiyo, Stanley Kevela alisema Manji alipewa siku 14 zilizoanza
kuhesabiwa tangu Jumamosi ili kulipa deni.
Alisema endapo siku hizo
zitamalizika bila kulipwa, mali za mfanyabiashara huyo zitakamatwa ili kufidia
deni la Dola 6.1 milioni za Marekani (zaidi ya Sh13 bilioni) anazodaiwa.
Kevela alisema fedha hizo ni
gharama ya kupanga kwenye jengo hilo ambalo ni mali ya Mfuko wa Pensheni wa
Watumishi wa Umma (PSPF).
Alisema baada ya kukamilika kwa
mchakato huo, kampuni italikabidhi jengo hilo kwa PSPF kwa ajili ya shughuli
nyingine.
Mfanyabiashara huyo alipotafutwa
jana ili kuzungumzia suala hilo, simu yake ya mkononi haikupatikana.
Mkurugenzi wa kampuni ya Yono, Skolastika
Kevela alisema kazi ya kuondoa mali za mpangaji kwenye jengo hilo ilikamilika
juzi.
“Kampuni zote zimeshaondoa vifaa na
milango ya jengo hilo imefungwa kwa kufuli za kampuni yetu. Tutalisimamia jengo
hadi tutakapowakabidhi PSPF,” alisema.
Uamuzi wa Manji kuhamishwa kwenye
jengo hilo ulitolewa na Mahakama kutokana na kushindwa kulipa kodi ya pango
ambapo alipewa masaa 24 ya kuondoa vitu vyake.
No comments:
Post a Comment