Kesi ya wizi wa simu aina ya Tecno
iliyochukua takriban miaka miwili mahakamani, imefika tamati kwa mtuhumiwa
kufungwa maisha jela.
Hukumu hiyo ilifikiwa jana katika
Mahakama ya Wilaya ya Ilala, baada ya mtuhumiwa Kassim Salum (18) kukutwa na
hatia kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu wa simu yenye thamani ya
Sh110,000.
Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa
hilo Januari 28, mwaka jana katika Mtaa wa Ghana Magenge eneo la Buguruni
jijini Dar es Salaam.
Ushahidi uliotolewa na mashahidi
watano uliiwezesha mahakama kukubaliana na madai ya mlalamikaji Lutifia
Mohamed.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi
wa mahakama hiyo, Flora Haule alisema, “Baada ya kusikiliza mashahidi
wote watano wa upande wa jamhuri, mahakama inaona wamethibitisha mashtaka dhidi
ya mshtakiwa.”
Akipitia ushahidi huo, hakimu Haule
alisema mshtakiwa alimsukuma mlalamikaji na kuangukia katika karai la mafuta
ambalo lilikuwa jikoni.
Mashahidi hao waliieleza jinsi
mshtakiwa alivyomvamia mlalamikaji akimtaka atoe simu aliyokuwa nayo na katika
purukushani hizo, alimpiga ngumi tumboni hali iliyosababisha kuishiwa
nguvu.
Ilielezwa kuwa kutokana na kupigwa,
mlalamikaji aliirusha simu upande wa pili ambapo kulikuwa na muuza chipsi,
hivyo Salum aliamua kumuachia mlalamikaji ili aende kuifuata.
Hata hivyo, wakati mlalamikaji
anajaribu kuokota simu yake, Salum alimsukuma akaangukia katika karai la mafuta
ya moto na kumsababishia kuungua eneo lote la mgongoni. Inadaiwa baada ya hapo
Salum alichukua simu hiyo na kutoweka nayo.
Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto
aliomba mahakama impe adhabu kali Salum ili aweze kujifunza kwa kuwa amemtia
mlalamikaji ulemavu wa kudumu.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mahakama ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea na Salum aliomba isimpe adhabu kali akisema si yeye aliyechukua simu hiyo, bali ni chuki binafsi za mitaani wanakoishi.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mahakama ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea na Salum aliomba isimpe adhabu kali akisema si yeye aliyechukua simu hiyo, bali ni chuki binafsi za mitaani wanakoishi.
No comments:
Post a Comment