JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha
linawashikilia watu 12, wakiwemo viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Mkoa wa Arusha.
Viongozi hao walikamatwa kwa amri
ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo wakituhumiwa kuhusika kuchoma moto
mashine za kuvuta maji kutoka kwenye chanzo cha Kangdet wilayani Karatu kwa
madai kwamba wanatekeleza agizo la Serikali, hatua ambayo imeelezwa kuwa
haikufuata utaratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana mjini Arusha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, aliwataja
waliokamatwa kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Karatu, Moshi
Darabe ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Barai, anayedaiwa kuhamasisha wananchi
kuchoma moto mashine hizo zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 16.
Wengine waliokamatwa ni Diwani wa
Kata ya Mang’ola, Lazaro Emanuel, viongozi wa vijiji vya kata hizo pamoja na
baadhi ya wananchi.
Kamanda Mkumbo alisema kuwa msako
wa kuwakamata watuhumiwa wengine waliohusika na tukio hilo bado unaendelea na
uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.
Desemba 27, mwaka huu, kundi la
wananchi wa vijiji vinne vya kata hizo waliandamana, wakang’oa na
kuchoma moto mashine za kuvuta maji katika chanzo cha maji cha Kangdet,
kinachotegemewa na vijiji vingine vya Kata ya Barai.
Kutokana na tukio hilo, Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa ikiongozwa na mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa
wa Arusha, Gambo, walitembelea eneo la tukio na baada ya viongozi kueleza
kilichotokea, aliagiza kukamatwa kwa watu wote waliohusika na uharibifu huo.
“Sheria lazima ichukue mkondo wake
kwani agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa lilikuwa wazi na halikusema wananchi
wachukue sheria mkononi, jambo hili ni kinyume cha sheria,” alisema Gambo
katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Karatu, Jubilate Mnyenye (Chadema), amesema kuwa yeye, mbunge wa jimbo hilo,
Willy Qambalo na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mang’ola, Jacob Pius, wametakiwa
kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi jijini Arusha leo asubuhi kwa mahojiano kuhusu
tukio hilo.
No comments:
Post a Comment