Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara
(Chadema) amepinga amri iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda ya wafanyabiashara kufunga maduka yao kila siku ya Jumamosi kuanzia saa
12 asubuhi hadi saa nne ili wafanye usafi.
Amesema amri hiyo ni batili na
haitekelezeki kwa sababu inarudisha nyuma uchumi wa wananchi hususani
wafanyabiashara ndogondogo ambao wanategemea kipato chao cha siku kuendesha
maisha yao.
Akizungumza na wananchi wa Mtaa wa
Kivule mwishoni mwa wiki, Waitara alisema yeye hapingani na watu kufanya usafi
katika maeneo yao, lakini amri ya kufunga maduka kila Jumamosi inaathiri uchumi
wa wananchi hivyo ni batili na haipaswi kuendelea kuwapo.
Siku chache baada ya kuteuliwa
kuongoza Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda alipiga marufuku kufungua maduka na
biashara zingine kabla ya saa nne asubuhi ili muda huo utumike kufanya usafi na
anayekaidi agizo hilo hutozwa faini isiyopungua Sh 50,000.
Mbunge huyo wa Ukonga alisema
uchumi wa watu masikini hususani wa mjini unategemea kile wanachokizalisha kila
siku, hivyo amri ya kufunga biashara kila wiki ni kurudisha nyuma juhudi za
wananchi kujiletea maendeleo yao.
Katika mkutano huo aliwaambia
wananchi hao kujiwekea utaratibu kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi wakati
wote na kila Jumamosi wafungue biashara zao asubuhi kama kawaida na
wasibughudhiwe na mtu yeyote.
“Mimi naunga mkono utaratibu wa
kufanya usafi kila mwezi uliotangazwa na Rais Dk. John Magufuli ambao upo kwa
mujibu wa taratibu, lakini huu wa kila Jumamosi mimi sina mwongozo nao na hizo
faini za kila wiki sizitambui na ni batili.
“Ninachotaka kila mtu afanye usafi
kwenye eneo lake, hizi faini zinatozwa bila utaratibu hata kama eneo la mtu ni
safi sitaki kuzisikia, wananchi hawa si wanyama, waelimishwe waachwe wajiwekee
utaraibu wao.
“Hivi mama, baba ntilie
anayepika maandazi, vitumbua, chapati afunge biashara tangu asubuhi mpaka
saa nne halafu hiyo chai itanywewa na nani, huyu mtu unamwambia afunge biashara
ili akaibe mtaani?” alihoji mbunge huyo na kuongeza:
“Watendaji lazima muwasikilize
watu, nasikia kinachofanyika ni mwendo wa kuviziana, waacheni watu wafanye
kazi, hapa ni kazi tu sio faini tu” alisema Waitara.
Katika hatua nyingine, Waitara
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule alivunja kikundi cha
ulinzi kilichokuwa katika ofisi hiyo kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya
rushwa pamoja na kuwanyanaysa wananchi.
Badala yake, alisema uitishwe
mkutano wa hadhara watu wote wanaohitaji kazi hiyo walete maombi katika ofisi
hiyo na baadaye wajadiliwe na wananchi katika mkutano wa hadhara ili kuepuka
kuwapa kazi watu wasiokuwa waaminifu katika jamii.
No comments:
Post a Comment