Katika hali isiyo ya kawaida
mzee mwenye umri wa miaka 75, Athuman Mchambua, mkazi wa Mtoni kwa Azizi Ally
jijini Dar es Salaam amezua gumzo mtaani baada ya kuamua kutafuta mke kwa
kuweka bango barabarani.
Katika bango aliloliweka katikati
ya barabara Mzee Mchambua alianisha sifa tano za mke anayemtaka pamoja na namba
za simu za kuwasiliana naye.
Sifa hizo ni pamoja na awe mshika
dini, uvumilivu wa ndoa, uwezo wa kilimo, apendo wa mume, watoto na wajukuu pamoja
na usafi wa hali ya juu.
Mzee Mchambua ambaye alizungumza na
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC Swahili) hivi karibuni alisema alifanya
uamuzi huo baada ya kufiwa na mke wake aliyezaa naye watoto 11 na kumwacha
akiwa hana mtu wa kumsaidia kutunza familia na kufanya shughuli za shambani.
Katika mazungumzo na mwandishi wa
BBC, alisema tayari wamejitokeza wanawake wanne waliotaka kuolewa naye lakini
hakuna hata mmoja aliyekidhi vigezo alivyoainisha.
Alisema alilazimika kutumia njia ya
tangazo kwa sababu anafiri kwa umri alionao hawezi kumpata mke kwa njia ya
kawaida.
Alisema endapo njia hiyo
itashindikana kumpata mke mwenye sifa anazotaka atalazimika kutumia madalali
kumsaidia kumtafuta mke mwenye sifa.
BBC pia ilizungumza na mmoja wa
watoto wa Mzee Mchambua, ambaye alisema anaona uamuzi wa baba yake ni sawa kwa
sababu ameweka sifa za mwanamke anayemtaka.
Mtoto huyo alisema wapo tayari
kumpokea mke mpya wa baba yao na watamheshimu kama mama yao mzazi.
No comments:
Post a Comment