Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo ‘Mzee wa
Upako’ baada ya kudaiwa kumfanyia fujo jirani yake ameendelea kujibu madai hayo
kwa mtindo wa ‘kudonoa donoa’ na jana aliwataka wanaodai kuwa alilewa siku hiyo
wataje alikunywa pombe gani na katika baa gani.
Wiki mbili zilizopita, taarifa kwenye vyombo vya habari zilisema
kwamba Mchungaji Lusekelo alikwaruzana na majirani zake huku akidaiwa kuwa
alikuwa amelewa jambo ambalo lilifanya achukuliwe na kuhojiwa na polisi.
Lakini, tangu kuibuka kwa tukio hilo alikataa kulitolea
ufafanuzi licha ya kutafutwa na vyombo vya habari, hata pale alipohudhuria
ibada kanisani kwake aliwaambia waumini wake hatalizungumzia na badala yake
alidonoadonoa baadhi ya matukio.
Alipokwenda kanisa kwake kwa mara ya kwanza Novemba 25,
Mchungaji Lusekelo alisema; “Kuna kitu nilikuwa nataka nikiseme, lakini
sitakisema ili waendelee kusema haohao waliokuwa wanasema.Wakawaulize wenyewe.
Nimeyaona magazeti hapa, ooh Mzee wa Upako, ooh Mzee wa Upako, sisemi. Sasa leo
yupo hapa, na kwa taarifa yao watashindana sana, lakini hawatashinda. Hii ni
kama kumpiga chura teke.”
Lakini, Novemba 28, Mchungaji huyo akajibu baadhi ya hoja
akisema kwanza, maneno aliyotumia ambayo ni mshenzi, mpumbavu na mjinga siyo
matusi kwani yameandikwa kwenye Biblia. Pili, watu hao ndiyo walianza kumtukana
yeye baada ya kuwauliza wanatafuta nini eneo la getini kwake.
Hoja nyingine alisema watu hao hawakuwa jirani zake kama
inavyodaiwa kwani mtaani kwake wanaishi kama majambazi kutokana na mazingira ya
kutofahamiana.
Jana, Mchungaji Lusekelo akiwahubiria waumini wake alidonoa tena
eneo jingine linalohusiana na tukio hilo, kwamba wanaodai alikuwa amelewa
pombe, waeleze alikunywa pombe gani na baa gani.
Akikaribishwa kwa wimbo wa kuabudu uitwao, ‘Nina haja nawe’
kabla ya kuanza kumtunza kwa sadaka, Mchungaji Lusekelo alisema watu
wanaotuhumu kuwa alilewa, wanatakiwa kueleza alikunywa pombe gani na alikunywa
akiwa eneo gani.
“Wiki iliyopita nilikuwa Wizara ya Mambo ya Ndani, baadhi ya
maofisa wakaniona , wewe Mzee wa Upako… Mzee wa Upako, askari mmoja akaniuliza
wewe Mzee wa Upako unachukua sadaka halafu unaenda kunywa pombe. Nikawauliza,
hiyo pombe nilikunywa wapi, halafu pombe zipo za aina nyingi, taja ni pombe
gani, ukienda mbali zaidi ungeuliza nililewa nini, maana hata upako wa roho
mtakatifu ni ulevi,” alisema.
“Lakini kuna majina ya watu, mitaani inaitwa pombe, sasa sijui
ni pombe gani hiyo….watashindana sana. Lakini kushindana siyo tatizo, je,
mtashinda? Eti oooh hayo maneno tu hata kwenye kanga yapo, subiri tusiandikie
mate na wino upo, ukitaka kummaliza Mzee wa Upako we mpige risasi tu,” alisema
huku akishangiliwa na waumini wake.
Alisema hakuna mwanadamu atakayeweza kumwangusha kwa
kipawa na kalama Mungu aliyompatia.
“Ndiyo maana unapojiita mtume leo unakuwa unajirusha kwenye
harakati ambazo zilijengwa na baba zetu, ndiyo maana kumshinda shetani ni
lazima, kuna mfumo umejengwa na mfumo huu uko imara kama chuma cha pua,”
alisema.
Katika ibada ya wiki iliyopita, mchungaji huyo alisema taarifa
zinazosambazwa kumchafua hazitamvunja moyo wa kuendelea kufanya kazi ya
uchungaji, huku akihoji kwanini magazeti yanaandika mabaya pekee na hayaandiki
habari za uponyaji anaofanya kanisani kwake.
No comments:
Post a Comment