Mfanyabiashara Yusuph Manji jana
alitii sheria bila shuruti kwa kuhama kwenye jengo la Quality Plaza akitekeleza
amri ya Mahakama ya kumtaka kurejesha jengo hilo ambalo ni mali ya Mfuko wa
Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF).
Mbali na kutekeleza amri ya kuhama
baada ya kupewa notisi ya saa 24 iliyomalizika juzi, pia anatakiwa kulipa
malimbikizo ya deni la pango la Dola za Marekani 6.1 milioni (zaidi ya Sh13
bilioni), ambazo kama asipozilipa mali zake zitakamatwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya
Mahakama Kitengo cha Ardhi kutoa hukumu ya kumtaka Manji kuondoka kwenye jengo
hilo pamoja na kuilipa deni la pango.
Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo,
Manji ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga hakupatikana kupitia simu yake ya
mkononi.
Viongozi wa kampuni za Manji
waliokuwa wakisimamia uondoaji wa vifaa uliomalizika jana asubuhi, walikataa
kuzungumza na waandishi wa habari waliofika kufuatilia tukio hilo.
Tangu juzi chini ya usimamizi wa
kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart, Manji na kampuni zake walikuwa
wanaondoa vifaa mbalimbali vilivyopo kwenye jengo hilo na kuhitimisha shughuli
hiyo jana.
Meneja Uendeshaji wa Yono Auction
Mart, Atukuzwe Mhugo alisema kampuni ambazo walikuwa wakizisimamia kuondoa
vifaa ni Quality Group Co Ltd, Gaming Managemeti Ltd, Q Consult Ltd na Quality
Logistics Co Ltd.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa
kampuni hiyo ya Yono, Scholastica Kenyela alisema tayari wameshaziondoa kampuni
za Manji kwenye jengo hilo.
Kenyela alisema mteja wao ambaye ni
PSPF alichukua uamuzi huo baada ya Manji kushindwa kulipa kodi ya pango ya
zaidi ya Sh13 bilioni.
“Sisi tumetimiza wajibu wetu, ukienda
pale utaona tayari tumeshafanya kazi yetu kwa sababu alipewa notisi ya saa 24
awe ameondoka,”alisema.
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa PSPF,
Abdul Njaidi alisema masuala yote yanayohusiana na jengo hilo kwa sasa yako
chini ya Yono Auction Mart. “Sipo Dar es Salaam na sitazung- umzia
chochote kuhusu jengo hilo wenye mamlaka ni Yono naomba uwatafute wao,” alisema.
No comments:
Post a Comment