WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mwigulu Nchemba ametaka apewe taarifa kuhusu taasisi na mashirika yasiyo ya
kiserikali (NGO) wanaohamasisha au kutangaza ndoa za jinsia moja nchini ili
azifutie usajili mara moja.
Aidha ametaka kutajwa kwa watu
wanaojihusisha na vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua za kisheria kwa
kujihusisha na vitendo hivyo ambavyo vinapigwa vita dunia nzima.
Nchemba aliyasema hayo jana mjini
Kibaha alipokuwa akizungumza na taasisi za Kijeshi za mkoa huo zikiwemo
Uhamiaji, Polisi, Magereza na Zimamoto juu ya kujua changamoto mbalimbali
zinazowakabili.
Alisema kuwa taasisi hizo hazifai
kwani zinafanya kazi ya laana ambayo ni kinyume cha maadili ya Kitanzania na
hazistahili kuendelea kufanya kazi kwa upotoshaji huo.
“Leteni majina ya taasisi hizo ili
tuzifute kwani hazistahili kuendelea kufanya jambo hilo ambalo ni laana na
halipaswi kufumbiwa macho ndani ya jamii,” alisema Nchemba.
Kamanda wa polisi mkoani Pwani
Bonaventura Mushongi alisema kuwa jeshi hilo linakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwa ni pamoja na upungufu wa vitendea kazi, ikiwa ni pamoja na
magari.
Mushongi alisema kuwa licha ya
kukabiliwa na changamoto hizo wamekuwa wakikabiliana na uhalifu kwenye mkoa huo
ambao umekuwa kimbilio la wahalifu kutoka mikoa jirani ya Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment