Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
ameiagiza Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu nchini (NBAA)
kuwachukulia hatua wale wote wanaoitia doa taaluma hiyo kwa kufanya ubadhilifu
wa fedha za umma.
Maagizo hayo yametolewa kwa niaba
yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mpango, wakati wa Uzinduzi wa Kituo
cha Taaluma ya Uhasibu (APC) uliokwenda sambamba na ufunguzi wa Mkutano wa
mwaka wa wahasibu unaojumuisha wadau kutoka nchi za Afrika Mashariki, katika
eneo la Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Amesema kuwa Idadi ya Wahasibu
wenye sifa inazidi kuongezeka na hivyo kuisaidia Serikali, japo kuwa Serikali
hairidhiki kuona wanataaluma wa Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu (CPA) wanaongezeka
huku vitendo vya ubadhilifu wa fedha za Umma na ufisadi vikiendelea kuripotiwa.
“Wapo hata wahasibu wanaotumia
taaluma yao vibaya, wanaowawezesha wafanyabiashara kukwepa kodi, wanachakachua
vitabu vya taarifa za fedha na kufanya ufisadi kwa njia ya kalamu na kompyuta
jambo ambalo halikubaliki hata kidogo” Aliongeza Dkt. Mpango
Alisema kuwa machozi ya masikini wa
Tanzania yatawafuata mafisadi hadi kaburini lakini serikali ya Awamu ya Tano
haitasubiri hao mafisadi wafe, itawatumbua na wala hakuna mzaha na kwamba
tayari mahakama ya mafisadi imeanza kazi na itawashughulikia.
Aidha, Waziri huyo wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango, amewaasa wanataaluma wa uhasibu na ukaguzi wa
hesabu kuitumia taaluma yao kuisaidia Serikali katika hatua yake ya kuelekea
katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda kwa kuwa taaluma hiyo ina umuhimu
mkubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji
wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu, Bw. Pius Maneno alisema
kuwa, Kituo hicho kilichozinduliwa cha APC hadi kumalizika, kitagharimu Sh.
Bilioni 35 ambapo mpaka sasa fedha zilizotumika ni takribani Sh. Bilioni 31.5.
“Gharama halisi za ujenzi wa kituo
hicho zilikuwa Bilioni 14 lakini kutokana na mzabuni wa ujenzi kuchelewesha
ujenzi ndio maana kumekuwa na Ongezeko la kiasi hicho cha fedha” aliongeza Bw.
Maneno.
Ujenzi wa kituo hicho ambao uko
katika eneo lenye ukubwa wa takribani ekari 14 umehusisha ujenzi wa Kumbi za
mikutano zinazochukua zaidi ya watu 1600, viwanja vya michezo na vyumba vya
kisasa 108 vya kulala wageni.
Bw. Maneno alisema kuwa kujengwa
kwa kituo hicho kutaifanya Bodi hiyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kilichokuwa
kikitumika kukodi kumbi za kufanyia na kusahisha mitihani ya Bodi (NBAA).
Alizitaja faida zingine kuwa ni
kuboreshwa kwa mazingira ya kitaaluma na wanataaluma wa uhasibu pamoja na
kuimarika kwa utawala bora na kuwa chachu ya uchumi wa viwanda, kwa kuwa Kituo
hicho, kinatoa elimu bora itakayowawezesha wahitimu kuingia kwenye ushindani
ndani ya nchi za Afrika Mashariki na Duniani kwa ujumla.
Ujenzi wa Kituo hicho umedhaminiwa
na serikali kupitia mkopo kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii-NSSF, Bodi ya
Uhasibu-NBAA na Mbia mwenza wa kituo hicho, Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa
Serikali-GEPF.
No comments:
Post a Comment