Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma
Kusini, David Kafulila, amesema atapokelea kadi ya Chadema jimboni mwake
baadaye mwezi huu.
Kafulila alitangaza kuhama
NCCR-Mageuzi na kurudi Chadema kwa alichoeleza kuwa ndicho chama
kilichojipambanua kuelekea safari ya mabadiliko ifikapo mwaka 2020.
Kada huyo tayari amewasilisha barua
kwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe kumjulisha kuwa anajivua
uanachama na anarudi Chadema.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi jana, Kafulila alisema ameamua kuwa atapokelea kadi hiyo jimboni kutokana
na mapenzi aliyonayo kwa wananchi wake.
"Nimepanga kuchukua kadi
mwezi huu jimboni, kwa kuwa ilikuwa nichukue kadi mwanzoni lakini ilishindikana
kutokana na siku kuu, hivyo siku yoyote kuanzia sasa nitachukua," alisema.
Wakati anajiuzulu NCCR-Mageuzi na
kurudi Chadema, alisema hakufanya uamuzi kwa kukurupuka bali alitafakari na
kushauriwa na wananchi wa jimbo lake, na kuridhika kurudi huko.
"Nilitafakari na kushauriwa
sana jimboni na kuridhika kwamba Chadema ndiko sehemu inayojipambanua kwa
mikakati ya kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania na ni vema kukusanya
nguvu ya kila mwenye kiu ya mabadiliko ndani ya chama kimoja, ili kufupisha
safari ya mabadiliko," alisema.
Alipoulizwa kwa nini amerudi
Chadema wakati aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Wilbrod Slaa
alipata kumwita sisimizi kwa alichoeleza kuwa hakuwa na imani naye,
alijibu kuwa siasa ni malengo si uhusiano binafsi.
Kafulila aliongeza kuwa wanasiasa wanaunganishwa
na malengo zaidi ya urafiki na kwamba malengo yake sasa ni kuendelea kupigania
mabadiliko ya kimfumo yanayoenea zaidi kwenye chama hicho (Chadema) kuliko
kingine.
Novemba 10, 2009 Kafulila alijivua
uanachama wa Chadema na kuhamia NCCR-Mageuzi kutokana na kuondolewa kwenye
nafasi ya uofisa habari wa chama hicho.
Pia akiwa NCCR-Mageuzi, alitimuliwa
uanachama kwa kudaiwa kukiuka taratibu za chama hicho na tuhuma za kutaka
'kumpindua' Mwenyekiti, James Mbatia.
Hata hivyo, suala hilo lilipata
suluhu baada ya Mbatia kuteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa Mbunge.
Wakiwa bungeni, Mbatia na Kafulila walikutana, kuzungumza na hatimaye kumaliza
mzozo wao.
No comments:
Post a Comment