WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amekagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA) Kanda ya Songea na kuagiza akiba ya mahindi iliyopo iendelee
kutunzwa hadi msimu ujao wa mavuno.
Ametoa agizo hilo jana jioni
(Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa NFRA
Kanda ya Songea pamoja na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma mara baada ya
kukagua akiba ya nafaka iliyomo kwenye maghala ya kituo hicho.
Waziri Mkuu alisema mabadiliko ya
tabia nchi yamefanya mvua zichelewe kunyesha katika mikoa mingi nchini ukiwemo
mkoa wa Ruvuma ambao kwa kawaida mwezi Januari mvua ya kutosha inakuwa
imeshanyesha na huwa kuna baridi nyingi.
“Angalieni ninyi wenyewe hali ya
joto iliyopo hivi sasa, kwa kawaida mvua ingeshaanza kunyesha mwezi huu na
mahindi yangekuwa yameanza kurefuka. Lakini hadi leo (jana) naambiwa mvua
imenyesha mara mbili tu na mahindi yaliyopandwa yameanza kunyauka.”
“Kama mvua haijanyesha hadi leo, ni
lazima tuchukue tahadhari, na hata mvua ikija hatujui itaendelea kunyesha hadi
lini na kwa kiasi gani. RC, Ma-DC na ma-DED toeni elimu kwa wananchi juu ya
utunzaji wa akiba ya chakula. Waambieni waachane na ngoma za unyago na sherehe
za kipaimara ambazo hutumia kiasi kikubwa cha chakula,”alisisitiza.
“Msiruhusu kutoa mahindi yaliyopo
na kuyauza. Hizo tani 10,500 zilizopo ziendelee kuhifadhiwa hadi tutakapoamua
vinginevyo,”alisisitiza.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa
NFRA Kanda ya Songea, Bw. Majuto Chabruma alimweleza Waziri Mkuu kwamba msimu
huu walipanga kununua tani 22,000 za mahindi kutoka kwa wakulima lakini hadi
kufikia Desemba 31, 2016, wamefanikiwa kununua tani 10,335.3 zenye thamani ya
sh. bilioni 5.28.
Alisema kanda ya Songea ni miongoni
mwa kanda saba zilizo chini ya NFRA ambayo inahudumia mkoa wa Ruvuma. Alizitaja
kanda nyingine zinazohudumia mikoa yote nchini kuwa ni Arusha, Kipawa, Dodoma,
Shinyanga, Makambako na Sumbawanga.
“Kanda ya Songea inayo maghala sita
yenye uwezo wa kuhifadhi ytani 29,000 za nafaka. Lakini hivi sasa kanda hii
imeingizwa kwenye Mpango wa Kuongeza Uwezo wa Hifadhi (NFRA Storage Expansion
Project) na lengo la Wakala ni kufikia uwezo wa kuhifadhi tani 700,000 ifikapo
mwaka 2020,” alisema.
“Kanda ya Songea tumenunua viwanja
viwili vyenye ukubwa wa mita za mraba 16,986 ambapo zitajengewa silos 12 zenye
uwezo wa kuhifadhi tani 46,000 na maghala mawili yenye uwezo wa kuhifadhi tani
5,000 kila moja na hivyo kuwa na ongezeko la tani 56,000 mradi huu
utakapokamilika.”
Alisema kukamilika kwa mradi huo,
kutaiwezesha kanda ya Songea kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 85,000 ndani ya
maghala na vihenge kutoka tani 29,000 za sasa.
Alipolizwa ni kwa nini hawajaweza
kutimiza tani zote walizojipangia kununua, Bw. Chabruma alisema kuimarika kwa
barabara za mkoa huo kumetoa changamoto kwa wakala kwani wananchi walianza
kuuza mahindi kabla ya msimu wa ununuzi haujaanza (kawaida ni Julai mosi kila
mwaka).
“Kuimarika kwa barabara za mkoa
kumesaidia kufungua biashara na mikoa ya jirani na hivyo kuwawezesha wakulima
wa Ruvuma kupata soko nje ya mkoa kabla NFRA haijaingia sokoni na kuanza
kununua nafaka kwa wakulima vijijini,” alifafanua.
Alisema changamoto nyingine
inayowakabili ni ubora hafifu wa nafaka kutoka kwa wakulima ambao alisema ni
tatizo tangu hatua za awali za uzalishaji wa mazao ya chakula na
biashara.
“Ubora hafifu wa zao la mahindi
ulionekana zaidi kwenye nafaka zilizooza, punje zilizovunjika, wadudu hai,
rangi mchanganyiko na takataka,” alisema.
Waziri Mkuu leo anatembelea wilaya
ya Songea na kukagua kituo cha kupoozea umeme katika kijiji cha Mtepa, atakagua
kituo cha afya cha Madaba ambako pia atazungumza na watumishi wa ummakatia
sekondari ya Madaba kabla kuhutubia mkutano wa hadhara. Pia atakagua shamba la
miti la TFS katika kijiji cha Wino.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI
MKUU
No comments:
Post a Comment