Kundi la al-Shabab nchini Somalia
limesema wapiganaji wake wameshambulia kambi ya wanajeshi wa Kenya wanaohudumu
chini ya kikosi cha Umoja wa Afrika (Amisom)nchini Somalia.
Wapiganaji hao wanadai kuwaua wanajeshi wengi kwenye shambulio
hilo katika kambi ya Kulbiyow kusini mwa Somalia karibu na mpaka wa nchi hiyo
na Kenya.
"Mujahideen (wapiganaji) wawili walivurumisha magari
yaliyokuwa na mabomu na kuyalipua kwenye lango la kambi hiyo ya mji wa Kulbiyow
kabla ya wapiganaji wengine kuingia. Baada ya makabiliano makali, tumefanikiwa
kuiteka kambi," mmoja wa wasemaji wa al-Shabab Sheikh Abdiasis Abu Musab
ameambia shirika la habari la Reuters.
Msemaji huyo amedai kundi hilo limewaua wanajeshi zaidi ya 50 na
kutwaa magari na silaha za wanajeshi hao, taarifa ambazo msemaji wa majeshi ya
Kenya amekanusha.
Kanali Paul Njuguna ameambia Reuters: "Ni uongo. Operesheni
ya kijeshi inaendelea. Tunaendelea kupokea taarifa."
Al-Shabab wamekuwa wakipigana dhidi ya serikali ya inayoungwa
mkono na mataifa ya magharibi na jamii ya kimataifa.
Wanajeshi wa Kenya pamoja na wanajeshi kutoka Djibouti, Uganda
na Ethiopia, chini ya Amisom, wamekuwa wakisaidia serikali hiyo yenye makao
yake Mogadishu.
Januari mwaka uliopita, wapiganaji wa al-Shabab walishambulia
kambi ya majeshi ya Kenya el-Adde na kuua wanajeshi wengi.
Al-Shabab walisema waliua zaidi ya wanajeshi 100. Jeshi la Kenya
halijatangaza idadi kamili ya wanajeshi waliouawa hadi wa leo.
No comments:
Post a Comment