Nachukua fursa hii kuwapongeza Sana
kwa kazi kubwa mliyoifanya kwenye chaguzi ndogo za udiwani na ubunge
zilizomalizika hivi punde nchi nzima. Ingawa hatukushinda hata kata moja katika
kata 20 zilizokuwa zinashindaniwa, lakini tumefanya vizuri kwenye matokeo.
Chama chetu kilisimamisha wagombea
katika Kata 5 kati ya Kata 20 nchi nzima, Isagehe (Kahama), Kijichi (Dar es
salaam), Kiwanja cha Ndege (Morogoro), Nkome (Geita) na Tanga (Songea). Na pia
tulisimamisha Mgombea katika Uchaguzi wa Ubunge Dimani (Zanzibar).
Baada ya kufanya kampeni kubwa
mzunguko wa kwanza tuliweza kutazama na kuamua kuwekeza kwa nguvu kwenye Kata
3.
Pamoja na kuwa hatukushinda Udiwani
wala Ubunge katika Uchaguzi , matokeo yameonyesha kukua kwa kasi kubwa kwa
Chama chetu. Tukishika nafasi ya 2 katika Kata ya Isagehe (Halmashauri ya Mji
wa Kahama) kwa kupata mara 2 ya Kura ya zile ambazo tulipata katika Uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015, hali hiyo ipo pia katika Kata ya Kijichi jijini Dar es
salaam na Nkome mkoani Geita.
Ni dhahiri kuwa sauti yetu
imesikika, Kampeni zetu zilizojikita juu ya masuala ya wananchi zimeleta
matunda kiasi.Nawapongeza sana viongozi wetu wa Chama katika Jimbo la Kahama
Mjini kwa kazi kubwa tulioifanya na kupiga hatua kubwa. Nawaomba wasikate Tamaa
bali wawekeze kwenye kuimarisha uongozi wa Chama Jimbo zima, kwenye kata zote
ili kuwa tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Katika Kata za Nkome mkoani Geita
na Kijichi mkoani Dar Es salaam tumefanya kazi kubwa Sana. Wagombea na viongozi
wetu wa Chama wa mikoa hii na kata hizi wamepigana kwenye mazingira magumu sana
ya ushindani mkali wa kisiasa. Kata hizi zimetupa fundisho kuwa wananchi
wanataka ushirikiano wa vyama vya upinzani. Ujumbe huo umefika na nawaomba
viongozi wetu wa Chama wajiandae kufanya kazi na vyama vingjne. Ubinafsi, roho
mbaya, chuki na kukomoana hakuwezi kutusaidia. Lazima tubadilike sisi wenyewe
kwanza kabla ya kutaka kuleta mabadiliko kwa wananchi.
Katika Kata ya Tanga Manispaa ya
Songea na kata ya Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro wanachama wetu na
viongozi walifanya kazi kubwa kuonyesha uwepo wa Chama kwenye maeneo yao.
Wamepanda mbegu za Chama na kwa uwezo wa mungu mbegu hizi zitamea na kuzaa
matunda.
Ni muhimu kukemea hali ya uchaguzi
ya Dimani, Naibu Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma – Zanzibar,
ndugu Seif Hamad, ni miongoni mwa waliojeruhiwa kutokana na kipigo baada ya
kutolewa Kituoni alipokuwa Wakala wa Chama kwa kupinga udanganyifu wa uchaguzi.
Bado uchaguzi kwa upande wa Zanzibar hauendeshwi katika misingi ya haki na
demokrasia.
Nawapongeza na kuwashukuru sana
wanachama wote wa ACT Wazalendo mliojitoa kwa Hali na Mali kushiriki kampeni
katika uchaguzi huu. Shukran za dhati Kabisa kwa madiwani wetu waliotumia
gharama zao kwenda kuishi vijijini kutafuta kura za Chama chetu. Sina cha
kuwalipa mungu atawalipa. Mmeonyesha mapenzi ya dhati kwa Chama chenu.
Mmeonyesha uzalendo wa dhati kwa vitendo.
Nawapongeza viongozi wa Chama wote
wakiwemo wale kwa Kitaifa kuanzia Mwenyekiti wetu – Mama Anna Elisha Mghwira,
Makamu Mwenyekiti – Mzee Shaaban Mambo, Kaimu Katibu Mkuu – ndugu Said Sanani,
na Naibu Katibu Mkuu – ndugu Msafiri Mtelemwa kwa kazi kubwa walioiafanya.
Nawapongeza pia makatibu wa Kamati za Makao Makuu ya Chama kwa kuwa waratibu wa
kata zilizoshiriki uchaguzi na kwa wale waliokuwa makao makuu kwa kufanya kazi
kubwa ya kuwasadia wenzao waliokuwa kwenye mapambano. Kwa Kweli tumefanya kazi
kama timu na sote tumechangia matokeo haya tuliyoyapata.
Uchaguzi umekwisha. Badala ya
kutumia muda wetu kujadili matokeo, tukubali tumeshindwa na kuanza kujipanga
kujenga Chama kwenye maeneo yetu. Tuwaunge mkono walioshinda lakini pia
tuwakosoe wanaposhindwa kuwajibika. Tusiache kuwasemea wananchi na kuhangaika
na changamoto zao za maisha – msingi wetu wa Siasa zinazojikita juu ya masuala
ya wananchi ni muhimu sana.
Ndio kazi yetu hii Kama Chama cha
siasa. Tulitumia fursa ya kampeni za chaguzi ndogo kupaza sauti kwenye masuala
ya kitaifa na tulifanikiwa Sana kwenye masuala mbalimbali na kutengeneza ajenda
za kitaifa. Tusichoke kuendelea kuwa Chama cha masuala na sio matukio. Chama
cha hoja Badala ya viroja. Chama cha UTU.
Tuendelee kutaka shughuli za
kisiasa kuendelea kwa mujibu wa Sheria. Tuendelee kulaani vikali uamuzi wa
Serikali kuzuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.
Ahsanteni Sana
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama (KC)
ACT Wazalendo
Januari 23, 2017
No comments:
Post a Comment