Mkazi wa Sitakishari Dar es Salaam,
Christina Thomas (28), amekataa kudhaminiwa ili arudi rumande na msichana wake
wa kazi ambaye alishindwa masharti ya dhamana.
Christina jana alifikishwa Mahakama
ya Wilaya ya Ilala kwa tuhuma za kumpiga mtoto wake wa miaka miwili na
kumsababishia majeraha makubwa, kuzimia na kushindwa kumpeleka hospitalini.
Mwendesha Mashitaka Hilda Kato,
alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ritha Tarimo kwamba
mshitakiwa siku isiyofahamika Januari, alimpiga kwa fimbo mtoto huyo na
kumsababishia majeraha.
Kato alidai katika mashitaka ya
pili, mshitakiwa huyo ambaye ni mama mzazi wa mtoto huyo na msichana wake wa
kazi, Blanka Benjamin kwa uzembe walimwacha mtoto huyo bila kumpeleka hospitali
huku akiwa na hali mbaya ambayo ilisababishwa na mama mzazi.
Baada ya kusomewa mashitaka, mama
huyo alijibu kuwa hakumbuki, huku mshitakiwa wa pili ambaye ni msichana wa kazi
akikana mashitaka yake.
Mwendesha Mashitaka alimwambia
Hakimu Tarimo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, lakini dhamana
yao iko wazi kama watakidhi masharti.
Hakimu alitoa masharti ya dhamana
kwa washitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika mmoja akiwa mtumishi
kwenye taasisi inayofahamika na kusaini dhamana ya Sh 800,000 kila mmoja.
Baada ya kusomewa masharti hayo ya
dhamana mshitakiwa namba moja alikidhi masharti ya dhamana huku wa pili
akishindwa kutokana na wadhamini kuchelewa.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo wa
kwanza ambaye ni mama wa mtoto alisema hawezi kuwa nje kwa dhamana akimwacha
mshitakiwa wa pili rumande hivyo kumwomba hakimu warudi wote ndani hadi kesho
watakapotimiza masharti ya dhamana pamoja.
Hakimu alimwambia mshitakiwa huyo
kwamba kwa sababu yeye ana mtoto mdogo hivyo angeweza kutoka na kumwacha
mshitakiwa wa pili na kesho (leo) angepata dhamana, lakini akasema mtoto wake
ataondoka na baba yake, na yeye atarudi rumande hadi watakapopata dhamana wote
wawili.
No comments:
Post a Comment