
RAIS John Magufuli amesema serikali
inawachunguza watumishi wa umma waliogushi umri ili wasibaki kwenye utumishi wa
umma kwa muda ambao hawakustahili kuwa kazini.
Kadhalika, amesema kuna watumishi
wenye miaka 60 na zaidi ambao hawataki kustaafu huku waking’ang’ania ajira na
madaraka, na wengine wakijipachika vyeo vya ukurugenzi.
Akizungumza katika sherehe za
maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) ambazo kitaifa
zilifanyika jana katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Rais
Magufuli alisema uchunguzi huo wa umri umeshaanza.
“Wako watumishi ambao wamebadilisha
umri wao," alisema Rais Magufuli. "Wamebadilisha miaka yao na unakuta
ni mzee kabisa, lakini kabadilisha umri.
"Kuna watu ambao ni wazee tena
kuliko mimi. Wanasema hawaondoki eti ndio wakati umefika, hao nao
tunawachunguza.”
Katika hotuba yake, Rais Magufuli
alisisitiza kuwa wapo watumishi wa umma ambao bado wanafanya kazi wakiwa
wameshatimiza umri wa kustaafu kwa lazima wa miaka 60 lakini hawataki kustaafu
ili kuachia nafasi wegine waajiriwe.
Watoto wa viongozi
Alisema katika watu walioghushi vyeti,
kuna baadhi ni watoto wa viongozi ambao walijipatia ajira bila uhalali huku
watoto wa maskini wamekuwa hawaendi kokote, licha ya kuwa na vyeti halisi.
Alisema kwa sababu hiyo serikali
ilisimamisha ajira kwa muda mrefu, kwa kuwa wafanyakazi walikuwa ni wengi
wakiwemo hewa na wenye vyeti vya kughushi.
Rais aliwahoji wafanyakazi, “Hivi
mlitaka nipandishe mishahara niwapandishie ndani humo na wale wafanyakazi hewa
na watu wa kughushi vyeti, ndio maana nilitaka kwanza nisafishe nyumba.
Alisema kwa sasa mwelekeo ni mzuri
na atakapopandisha mshahara atafanya hivyo kwa watumishi sahihi na ndio nia ya
serikali.
Alisema wafanyakazi hewa, sio jipu
maana halionekani, ila wafanyakazi wenye vyeti feki wapatao 10,000 ndio majipu
na ameamua kuwatumbua, maana ndio walikuwepo. Alisema ameshaagiza watu wote
ambao wameorodheshwa kwenye orodha ya vyeti feki, wajiondoe ndani ya siku 15.
“Waondoke hata kama ni mtoto wa
waziri au wa rais, yeyote anayehusika aondoke. Akigoma apelekwe mahakamani na
huko najua kifungo chao sio chini ya miaka saba,” alisema
Rais Magufuli.
Hata hivyo, alisema kwamba
anachojua, watumishi hao wenye vyeti feki watajiondoa tu wenyewe kwa kuwa
mishahara hawataendelea kupata.
Rais Magufuli alisisitiza kuwa
viongozi wa juu, hawana nia mbaya kufanya uhakiki huo, bali wana nia nzuri,
kwani wanataka watumishi ambao wanadai maslahi yao yaboreshwe, yaende kwa watu
sahihi.
Rais Magufuli alisema serikali
inataka kila kazi iwe na mfanyakazi mwenye sifa stahiki na kama ni ya darasa la
saba, afanye mtu mwenye elimu hiyo na sio kughushi cheti.
Alisema serikali imefanya uhakiki
huo ili kama ni mtu wa darasa la saba, aombe kwa sifa ya cheti chake na sio
kwenda kufoji cheti cha kwenda kufanya kazi ya uuguzi wakati hajafikia sifa
hiyo.
Rais alisema kuna wakurugenzi wa
mashirika na taasisi za serikali ambao wameghushi vyeti, halafu wanawanyanyasa
watu wa chini ambao hawana vyeti vya kughushi. Alisema watu hao walioghushi,
hawastahili nafasi hizo na ndio maana Serikali imeamua kuwaondoa.
No comments:
Post a Comment